Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WAZIRI MKUU ATOA WITO KWA WANAMICHEZO KUDUMISHA MAZOEZI KWA AJILI YA AFYA

Imewekwa: 16 Nov, 2026
WAZIRI MKUU ATOA WITO KWA WANAMICHEZO KUDUMISHA MAZOEZI KWA AJILI YA AFYA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amewahimiza wanamichezo kutoka taasisi zaidi ya 89 zinazoshiriki mashindano ya SHIMMUTA kuendelea kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, akieleza kuwa michezo ni sehemu muhimu ya kulinda afya, kuimarisha uimara wa mwili na kuzuia magonjwa mbalimbali.

Waziri Mkuu ameyasema hayo Novemba 12, 2026, katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro wakati anafungua rasmi Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Kampuni Binafsi Tanzania (Shimmuta). Waziri Mkuu amesisitiza kuwa ushiriki katika michezo haupaswi kuishia kwenye mashindano pekee, bali unapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa watumishi, ili kuwawezesha kuwa na afya bora, kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi na kujenga mshikamano baina ya taasisi.

“Michezo ina nafasi kubwa katika kuimarisha afya ya mwili na akili, hivyo ni muhimu kwa watumishi kutumia fursa zinazotolewa na mashindano ya SHIMMUTA kuendeleza vipaji vyao huku wakizingatia umuhimu wa mazoezi katika maisha yao ya kila siku”, alisisitiza Dkt. Nchemba.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkemia Mkuu wa Serikali, Benny Mallya amewapongeza Wachezaji wa Timu ya GCLA Sports Club kwa kujitokeza kushiriki mashindano hayo na kuonesha uzalendo kwa Mamlaka kupitia michezo. Alisema ushiriki wao katika SHIMMUTA ni sehemu ya kuimarisha mshikamano, ushirikiano na kujenga taswira nzuri ya Mamlaka, huku akiwahimiza kuendelea kupambana kwa bidii, nidhamu na kujituma ili kuhakikisha wanafikia malengo ya ushindi.

Wachezaji wa GCLA Sports Club wameendelea kuonesha dhamira ya kulitangaza vema jina la Mamlaka kupitia mashindano hayo, huku wakiahidi kuendelea kupambana katika michezo mbalimbali ili kupata matokeo chanya.