Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

Utangulizi &Majukumu Mahsusi

1.HISTORIA

Mamlaka ya Mabaara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS) ilianzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na.8 ya Mwaka 2016.Pamoja na majukumu mengine, Sheria ya Mamlaka inaipa jukumu Mamlaka ya kuwa chombo cha juu na Maabara ya Rufaa katika masuala yote yanayohusu uchunguzi wa sayansi jinai na huduma za vinasaba, ubora wa bidhaa na usimamizi wa kemikali. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imepitia mabadiliko mbalimbali kutoka kuwa Idara ndani ya Wizara, Wakala kati ya mwaka 1999-2016 na kuwa Mamlaka kuanzia tarehe 5 Aprili,2017 hadi sasa. Kihistoria Mamlaka hii ilianza kama kituo cha kufanya utafiti wa magonjwa ya ukanda wa joto kwenye maabara ya taifa mwaka wa 1895 na baadae kuhamishiwa Wizara ya Afya baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1947.

Kati ya mwaka 1947-1959 Maabara ilihamishiwa Wizara ya Kilimo na Maliasili na kutoka mwaka 1958 hadi sasa Maabara ipo chini ya Wizara yenye dhamana ya Afya. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa Mamlaka imeimarisha utekelezaji mzuri wa majukumu yake, kufikiwa kwa malengo, dhima na dira yake, hivyo kuchangia jitihada za Serikali katika kuboresha ustawi wa watu wake na mazingira

2.MAJUKUMU MAKUU

Majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni kama yalivyoorodheshwa chini ya Sheria ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na. 8 ya Mwaka 2016. Majukumu hayo ni:

  • Kufanya shughuli za utafiti, uchunguzi wa maabara na kutoa ushauri kwa Serikali kwenye masuala yanayohusiana na uchunguzi wa sayansi jinai toksikolojia, sayansi jinai baiolojia na vinasaba, sayansi jinai kemia, vyakula, dawa usalama mahali pa kazi, kemikali za viwandani na bidhaa zake na sampuli za mazingira kwa ajili ya kutekeleza afua za afya, sheria, ustawi wa jamii na mazingira;
  • Kuanzisha, kusimamia na kudhibiti uendeshaji wa Kanzidata ya Taifa ya Vinasaba vya Binadamu kwa mujibu wa Sheria ya Vinasaba, Sheria ya Mamlaka na Sheria;
  • Kuratibu Programu za Taifa za usimamizi wa kemikali, sayansi jinai na huduma za vinasaba;
  • Kusimamia Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Sumu;
  • Kusimamia na kuendesha mafunzo na programu za Elimu kwa Umma katika masuala yanayohusiana na usimamizi wa kemikali, huduma za vinasaba na masuala mengine yanayosimamiwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na. 8 ya Mwaka 2016;
  • Kutengeneza na kutoa mwongozo, maelekezo,fursa, mafunzo na kuwaandaa wanasayansi ndani na zaidi ya utaalam wa majukumu ya Mamlaka;
  • Kukusanya kutambua na kuchunguza kisayansi vielelezo vinavyohusiana na masuala ya kisheria;
  • Kusajili, kusitisha au kufuta maabara za kemikali, sayansi jina na vinasaba vya binadamu;
  • Kusajili, kusitisha au kufuta kemikali za viwandani, kemikali za majumbani au wadau wa kemikali;
  • Kufuta vibali vya utafiti au leseni za Vinasaba;
  • Kubatilisha na kutoa maelekezo au uteketezaji wa vitu, kemikali na mazao ya kemikali;
  • Kumshauri Waziri kuhusu uteuzi wa wakaguzi, maafisa uchukuaji sampuli na wachunguzi wa maabara wa serikali
  • Kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa maabara
  • Kuchukua sampuli na kufanya uchunguzi kwenye masuala yenye maslahi ya kitafia au umma au jamii kwenye uchunguzi wa sayansi jinai, ubora wa bidhaa na usimamizi wa kemikali kadri itakavyohitajika;
  • Kufanya ukaguzi kwenye maeneo au huduma zinazosimamiwa na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali
  • Kutekeleza majukumu mengine yoyote kama atakavyoelekeza Waziri.