Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MSHIKAMANO YAENDELEA KUIPA GCLA USHINDI SHIMMUTA

Imewekwa: 16 Nov, 2026
MSHIKAMANO YAENDELEA KUIPA GCLA USHINDI SHIMMUTA

Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Evaclotida Kapinga amesema umoja, mshikamano, nidhamu, kujituma na ushirikiano kati ya wachezaji ni miongoni mwa siri kubwa zilizochangia mafanikio ya timu ya mpira wa pete ya Mamlaka ambayo imeonesha ushindani na kufanya vizuri katika mashindano ya SHIMMUTA 2026 mkoani Morogoro.

Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya DIT katika viwanja vya Shule ya Sekondari Morogoro Novemba 8, 2026, Mkurugenzi ambaye pia ni mchezaji wa timu ya mpira wa pete ya GCLA Queens, amesema kuwa ushindi uliopatikana uwanjani si matokeo ya juhudi za mchezaji mmoja mmoja, bali ni matokeo ya maandalizi mazuri, nidhamu, kuaminiana na kucheza kwa ushirikiano kama timu moja.

“Siri kubwa ya ushindi wetu ni umoja, ushirikiano na nidhamu. Mpira wa pete ni mchezo unaohitaji kila mchezaji kutimiza wajibu wake na kumwamini mwenzake. Hatuwezi kupata ushindi kama kila mmoja atacheza kwa uwezo wake bila kuzingatia ushirikiano wa timu nzima. Tunahakikisha tunasikiliza maelekezo ya mwalimu na kutumia kila nafasi tunayopata uwanjani,” alisema Evaclotida.

Aidha, ameongeza kuwa siri nyingine ya mafanikio yao ni kufuata maelekezo ya mwalimu, kuheshimu majukumu ya kila mchezaji na kuwa na dhamira ya pamoja ya kuhakikisha timu inafikia malengo iliyojiwekea katika kila mchezo.

Aliongeza kuwa michezo ya SHIMMUTA imekuwa fursa muhimu kwa watumishi kuonesha vipaji vyao, kujenga afya bora, kukuza mshikamano na kuimarisha mahusiano baina ya watumishi wa taasisi mbalimbali za Serikali.

Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa watumishi wote wa GCLA kuendelea kuwaunga mkono wachezaji wa timu mbalimbali zinazoliwakilisha Mamlaka katika mashindano ya SHIMMUTA, kwa kutoa hamasa, sapoti na kuwaombea timu hizo ili ziendelee kufanya vizuri na kuiletea Mamlaka heshima.

Amesisitiza kuwa sapoti ya watumishi ni sehemu muhimu ya mafanikio ya timu, kwani huwapa wachezaji nguvu ya kujiamini, ari ya kupambana na moyo wa kutokata tamaa wanapokuwa katika mazingira ya ushindani.

Kwa upande wake, mwalimu wa timu ya mpira wa pete ya GCLA, Memick Mollel amesema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika michezo iliyopita, bado kuna maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili kuhakikisha timu inafanya vizuri zaidi katika mashindano.

Pia, ameeleza kuwa mipango iliyopo ni kuendelea kuboresha mbinu za uchezaji, kuongeza mazoezi ya kiufundi na kimwili, kuimarisha mawasiliano baina ya wachezaji pamoja na kufanya tathmini ya changamoto zilizojitokeza katika michezo iliyopita ili kuzifanyia kazi.

Aidha, amesema kuwa maandalizi hayo yanalenga kuhakikisha wachezaji wanaingia katika michezo wakiwa na utimamu wa mwili, utayari wa kisaikolojia na uelewa mzuri wa mbinu za mchezo, huku akisisitiza umuhimu wa nidhamu na kujituma kwa kila mchezaji kwani matarajio ya benchi la ufundi ni kuona timu ikiendelea kupiga hatua, kuongeza ushindani na kutumia kila mchezo kama fursa ya kujifunza na kuboresha kiwango chake.