Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WAJASILIAMALI WAPEWA ELIMU YA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI

Imewekwa: 16 Nov, 2026
WAJASILIAMALI WAPEWA ELIMU YA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI

Meneja Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa, amewataka Wajasiriamali wadogo na wa Kati kuzingatia matumizi salama ya kemikali katika shughuli zao za ujasiriamali kwa kufuata taratibu na miongozo inayotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kulinda afya za binadamu na mazingira.

Danstan Mkapa, ameyasema hayo Novemba 12, 2026 wakati wa mafunzo ya Uhifadhi na matumizi salama ya Kemikali kwa Wajasiriamali wadogo na wa Kati, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Niwaombe mzingatie sehemu mnayohifadhia kemikali iwe sehemu salama ili kuepusha ajali za kumwagikiwa na kemikali na pia kwa lengo la kuwalinda wengine wanaotuzunguka katika mazingira ya  nyumbani, bila kusahau kutumia vifaa kinga pindi mnaposhughulika na kemikali ili kujilinda dhidi ya athari za kemikali. Kwa kufanya hivyo tutaweza kujiepusha na madhara ya kemikali yasiyo ya lazima,” alisema Mkapa.

Aidha, Danstan Mkapa, amewaomba Wajasiriamali waendelee kutoa ushirikiano na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pindi wanapokumbana na changamoto katika matumzi ya kemikali, pia katika suala zima la uteketezaji wa mabaki na vifungashio vya kemikali viteketezwe kwa kufuata utaratibu husika wa uteketezaji ili kulinda mazingira na afya za wanajamii.

Kwa upande wa Wajasiriamali, Adili Suleiman na Anna Ibrahimu, walitoa shukrani kwa Ofisi ya Kanda ya Mashariki na Mamlaka kwa ujumla, kwa kuwapatia mafunzo kwa sababu wamepata fursa za kujifunza umuhimu wa kuzingatia kanuni na taratibu za alama wanapotumia kemikali ikiwemo utambuzi wa kemikali, namna sahihi ya kuzitumia, kuzihifadhi na kuchukua tahadhari dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kusababisha madhara kwa afya ya jamii na mazingira.

“Tunashukuru kwa mafunzo haya kwani yametufungua macho na kuongeza uelewa wetu kuhusu matumizi na uhifadhi salama kwa kemikali kwa sababu tumekua tukitumia baadhi ya kemikali katika shughuli zetu bila kufahamu kikamilifu tahadhari zinazopaswa kuzingatiwa,” walisema Wajasiriamali hao.

Aidha, Msimamizi wa Dawati la Usajili na Vibali vya Kemikali, Leocardia Magere, amewataka Wajasiriamali wadogo na wa Kati, kuhakikisha wanatumia kemikali zilizosajiliwa na zilizoruhusiwa kisheria, huku wakizingatia taratibu za usalama katika ununuzi, uhifadhi, matumizi na uteketezaji wa kemikali hizo.

“Ni muhumu kwa kila Mjasiriamali kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu kemikali anazotumia katika shighuli zake na pia kuhakikisha kemikali mnazotumia zimesajiliwa, hii inatusaidia kuepusha kutumia kemikali zisizotambulika na zisizo na lebo,” alisema Magere.

Aliongeza kuwa ni wajibu wa kila Mjasiriamali kuhakikisha anatumia vifaa kinga katika shughuli zake kwani hatua hii ni muhimu kwa sababu utoaji wa elimu hiyo ni jitihada za kuimarisha uelewa wa usimamizi na matumizi salama ya kemikali ikiwa njia ya kuwajengea uwezo wa kufanya shughuli zao za kiuchumi katika mazingira rafiki na salama zaidi.