Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WANANCHI WAKARIBISHWA KUPATA ELIMU NANENANE

Imewekwa: 11 Aug, 2026
WANANCHI WAKARIBISHWA KUPATA ELIMU NANENANE

Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Elias Mulima anawakaribisha wananchi kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya kutembelea banda la Mamlaka hiyo katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane 2026 yanayoendelea kwenye Viwanja vya John Mwakangale, mkoani Mbeya ili kupata elimu, ushauri wa kitaalamu na kufahamu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka katika kuhakikisha matumizi salama ya kemikali kwa maendeleo ya sekta za kilimo, mifugo na mazingira.

Akizungumza kuhusu maonesho hayo yaliyobebwa na kauli mbiu "Tambua Soko, Ongeza Tija, Kutekeleza Dira 2050," Meneja amesema Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inaunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo kwa kuhakikisha kemikali zinazotumika zinatumika kwa usalama, ufanisi na kwa kuzingatia sheria, kanuni na viwango vinavyotakiwa ili bidhaa za Tanzania ziweze kushindana katika masoko ya ndani na kimataifa.

"Tunawakaribisha wananchi wote kutembelea banda letu ili wapate elimu na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wetu. Kupitia maonesho haya, wananchi watajifunza namna sahihi ya kutumia na kuhifadhi kemikali pamoja na kuelewa huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka ambazo zinachangia kuongeza tija ya uzalishaji na kuhakikisha bidhaa zetu zinakidhi mahitaji ya soko, sambamba na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," alisema Mulima.

Meneja aliongeza kuwa wakulima watapata elimu kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu, mbolea na kemikali nyingine za kilimo kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa ili kuongeza uzalishaji, kupunguza hasara, kulinda afya za watumiaji na kuhakikisha mazao yanakuwa salama na yenye ubora unaokubalika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Aliongeza kwa kusema Maonesho ya Nanenane ni jukwaa muhimu linalowakutanisha wakulima, wafugaji, watafiti, wafanyabiashara, wanafunzi, wadau wa maendeleo na taasisi mbalimbali za Serikali, hivyo ni fursa adhimu kwa Mamlaka kuendelea kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya kemikali na mchango wake katika kulinda afya ya jamii, mazingira na kukuza uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake Obadiah Mwaikokesya, mkazi wa Tukuyu alisema elimu aliyopata imemsaidia kuelewa umuhimu wa kutumia na kuhifadhi kemikali kwa usahihi, akibainisha kuwa maarifa hayo yatamsaidia kulinda afya ya familia yake na kuongeza tija katika shughuli zake za kilimo.