DKT. NCHIMBI: WAFUGAJI BORESHENI MIFUGO ILI KUPANUA WIGO WA SOKO
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuendelea kuwasisitiza wafugaji kuboresha Mifugo yao ili kupanua wigo wa soko la mazao ya Mifugo ndani na nje ya nchi.
Balozi Dkt. Nchimbi aliyasema hayo Agosti 3,2026 wakati wa ziara yake kwenye mnada wa Mifugo uliopo kwenye viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma.
“Changamoto kubwa ni ubora wa mifugo yenyewe maana hata ukiwa na mifugo mizuri pia inahitaji masoko ili kuleta tija, Tufanye ufugaji unaozuia mifugo kuzurura tutumie njia za kitaalamu kufanya ufugaji huku tukijikita kuzalisha bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya soko” alisema Balozi Dkt. Nchimbi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani alisema kuwa moja ya vitu ambavyo Wizara yake imejielekeza kwa sasa ni upatikanaji wa mbegu bora za mifugo ambazo anaamini zitakuwa na tija kwa mfugaji ambapo zitawafanya kuwa na mifugo michache yenye uzalishaji mkubwa.
Baadhi ya Wafugaji akiwemo Juma Mapula na Machia Kasase wamesema ufugaji wa Kisasa unaongeza tija kwa kuongeza kipato na uhakika wa masoko kuliko ufugaji holela
“Zamani tulikuwa tunajifugia tu kwa sasa tunafuga kwa malengo na kuzingatia soko linataka nini imekuwa rahisi kutengeneza faida na bidhaa zinauzika japo kwetu tunahitaji nguvu ya namna ya kupenya kwenye soko la Kimataifa hasa kwenye bidhaa ya ngozi na Nyama” walisema.
Maonesha haya yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malecela yalikuwa na kaulimbiu ya “Tambua, Soko, Ongeza Tija, Kutekeleza Dira 2050”.