SEKTA YA KILIMO NA UVUVI KUFUNGUA FURSA ZA AJIRA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Sekta ya Kilimo na Uvuvi zimeendelea kuwa muhimu kwa kutengeneza fursa za uchumi na ajira nchini
Dkt. Samia amesema hayo Agosti 8, 2026 wakati akifunga maonesho ya Nanenane katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Dodoma.
“Serikali imeendelea kuwezesha Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuwezesha shughuli hizo nchini, miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuongeza bejeti ya wizara kilimo kufikia Trilioni 1.4 huku Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufikia Bilioni 174.6, Serikali itaendelea kutafuta masoko ya ndani na Nje ya Nchi kwa ajili ya mazao ya Kilimo Ufugaji na Uvuvi ili kuongeza tija” alisema Dkt. Samia
Aidha Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo amesema Wizara hiyo imeanza utekelezaji wa mpango wa kutafuta masoko ya kimkakati ya mazao ambayo hayajawekewa utaratibu kama mahindi na mpunga ili kuwanufaisha watanzania.
“Ulituagiza kutafuta masoko ya kimkakati ambayo hayajawekewa utaratibu kama mahindi na mpunga tumetambua maeneo kama Mbeya, Njombe, Songwe na Rukwa kama maeneo ya Ghala la Taifa na tumejipanga kushirikiana na Wataalamu kupunguza changamoto ya Sumu kuvu” alisema Chongolo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema Mkoa wa Dodoma unaendelea kupiga hatua katika sekta ya kilimo ikiwemo uanzishwaji wa kilimo cha zao la Apple ili kuinua uchumi wa wakazi wa Dodoma.
“Kwenye nchi yetu hakuna zao la Apple ili kuinua uchumi binafsi tumekuja na mpango wa zao mbadala tumefanya tafiti na tumegundua zao la Apple linakubali Dodoma na tumepata mbegu za aina tatu, mpaka sasa tayari kila wilaya ina shamba darasa la zao hili” alisema Senyamule.
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeshiriki maonesho hayo na kutoa Elimu kwa wadau 676 waliotembelea Banda Hilo.