Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WAGANGA WA TIBA ASILI WATAKIWA KUPIMA DAWA ZAO

Imewekwa: 02 Oct, 2026
WAGANGA WA TIBA ASILI WATAKIWA KUPIMA DAWA ZAO

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imetumia Maonesho ya 9 ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini upimaji wa dawa ni muhimu pia kwa sababu mwili wa mtu unaweza kuitikia dawa fulani tofauti na mtu mwingine, hivyo ni muhimu kwa watengenezaji na watoa tiba kufahamu viambata vilivyomo kwenye dawa zao ya Madini yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Geita, kutoa elimu kwa wadau wa madini na tiba asili kuhusu umuhimu wa upimaji wa dawa na kemikali ili kuhakikisha usalama, ubora na matumizi sahihi ya bidhaa hizo.

Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda ya Ziwa, John Wanjala, amesema maonesho hayo yamekuwa fursa muhimu kwa Mamlaka kukutana na wadau mbalimbali, wakiwemo wachimbaji wa madini, wafanyabiashara na waganga wa tiba asili, na kuwapatia elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

“Maonesho haya yametupa fursa kubwa ya kuwafikia wadau mbalimbali na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi salama ya kemikali na dawa asili. Tunawaeleza pia waganga wa tiba asili umuhimu wa kupima dawa zao ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya ubora na usalama. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pia inaendelea kutoa elimu kuhusu usindikaji bora na salama wa dawa asili, ili bidhaa zinazozalishwa nchini ziwe na ubora unaokubalika na ziweze kushindana katika soko la ndani na la kimataifa” alisema Wanjala.

Kwa mujibu wa Wanjala, hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza thamani ya dawa zinazozalishwa nchini na kuhakikisha zinakuwa na ubora unaoweza kuaminika na kukubalika katika masoko mbalimbali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mkoa wa Tiba Asili Geita, Mohamed Hamisi, maarufu Dk. Supu ya Mamba, amesema ushirikiano kati ya waganga wa tiba asili na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali umeleta mabadiliko katika dawa asili zinavyotengenezwa na kutumika, tofauti na zamani ambapo baadhi ya waganga walitengeneza dawa bila kujua kwa undani viambata vilivyomo na madhara yanayoweza kujitokeza, sasa wamekuwa na fursa ya kupata taarifa za kisayansi kupitia vipimo vya maabara.

“Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imetusaidia sana kutambua dawa zetu zina viambata gani, zina kiwango gani cha sumu na kama zinaweza kusababisha madhara kwa mtumiaji. Hii imetusaidia kuboresha tiba zetu na kutoa huduma kwa kujiamini zaidi,” alisema Hamisi.

Hamisi amewahimiza waganga wa tiba asili kutumia huduma za Mkemia Mkuu wa Serikali kupima dawa zao ili kupata taarifa sahihi kuhusu ubora na usalama wake kabla ya kuwapatia wananchi. Alipongeza huduma za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuendelea kusogezwa karibu na wananchi kupitia ofisi za kanda na madawati katika baadhi ya mikoa, hatua inayorahisisha wananchi na waganga kuwasilisha sampuli zao bila kulazimika kufika Makao Makuu.

Maonesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini yanafanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Geita, yakilenga kuwaunganisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini na kuwapa fursa ya kupata elimu, huduma na teknolojia zinazohusiana na shughuli za madini.