GCLA YAPONGEZWA KWA KULINDA AFYA, USALAMA WA WACHIMBAJI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (Mb), ameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kwa kushiriki katika Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.
Mhe. Sangu ametoa rai hiyo Septemba 24, 2026, alipotembelea banda la GCLA katika maonesho hayo, ambapo alieleza kuwa udhibiti na matumizi salama ya kemikali ni muhimu katika kulinda afya na usalama wa nguvu kazi ya Watanzania, hususani vijana wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini.
“Taasisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni taasisi muhimu sana katika kulinda nguvu kazi ya Watanzania, hasa katika udhibiti wa masuala ya kemikali. Nawapongeza pia kwa ushiriki wenu katika maonesho haya ya teknolojia ya madini, kwa sababu shughuli zote za uchimbaji wa madini kuna mahali kemikali zinahitajika kwa kiasi kikubwa. Kemikali hizi zisipodhibitiwa zinaweza kuwa na madhara kwa binadamu, hasa vijana wetu wa Kitanzania wanaofanya kazi migodini,” alisema Mhe. Sangu.
Aidha, Waziri Sangu alisema ushiriki wa GCLA katika maonesho hayo unaonesha umuhimu ambao Serikali inaupa udhibiti wa kemikali katika sekta ya madini, akibainisha kuwa sekta hiyo ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayohitaji uangalizi katika kuhakikisha kemikali zinatumika kwa usalama na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Alisema hatua hiyo pia inaendana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, hususani katika kujenga nguvu kazi imara na salama pamoja na kuwezesha maendeleo ya jamii.
“Niwapongeze sana na muendelee na ushirikiano huu na sekta ya madini. Lakini nitoe rai kuwa mtoe elimu. Mnajua nchi yetu Mwenyezi Mungu amebariki kwa rasilimali nyingi za madini na kumeibuka wimbi kubwa la wachimbaji wadogo ambao wanahitaji elimu, hasa katika matumizi salama ya kemikali,” alisema.
Mhe. Sangu alisisitiza kuwa wachimbaji wadogo wanapaswa kupewa elimu ya kutosha kuhusu matumizi sahihi na salama ya kemikali kutokana na nafasi kubwa ya shughuli za madini katika kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania, hususani katika mikoa inayozalisha madini kama Geita.
Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Mamlaka, Faustine Wanjala, alisema Mamlaka hiyo ina nafasi muhimu katika sekta ya madini kutokana na matumizi ya kemikali yanayohitajika katika shughuli mbalimbali za uzalishaji wa madini.
Alisema GCLA inatekeleza majukumu mbalimbali katika kuhakikisha matumizi ya kemikali yanafanyika kwa usalama, ikiwa ni pamoja na kutoa vibali, kusajili na kukagua wadau wanaojishughulisha na kemikali, pamoja na kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi na salama ya kemikali.
“Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni mdau mkubwa katika sekta ya madini, kwa sababu ili kuweza kupata madini ni lazima matumizi ya kemikali yatumike. Mkemia Mkuu wa Serikali anatoa vibali, anasajili na kukagua wadau wote wanaojishughulisha na shughuli za kemikali, lakini pia anatoa elimu kuhusu matumizi sahihi na salama ya kemikali ili zitumike katika uzalishaji huku watumiaji na jamii inayowazunguka wakiwa salama,” alisema Wanjala.
Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanafanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, yakishirikisha taasisi na wadau mbalimbali wa sekta ya madini. GCLA inashiriki katika maonesho hayo kwa kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu majukumu yake, udhibiti wa kemikali pamoja na matumizi salama ya kemikali katika shughuli za madini.