Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

GCLA YAWATAKA WACHIMBAJI KANDA YA KUSINI KUZINGATIA USALAMA WA KEMIKALI

Imewekwa: 01 Oct, 2026
GCLA YAWATAKA WACHIMBAJI KANDA YA KUSINI KUZINGATIA USALAMA WA KEMIKALI

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Kusini imewataka wachimbaji wa madini wakubwa na wadogo katika Kanda hiyo kuzingatia matumizi salama ya kemikali wanazotumia katika shughuli za uchimbaji na uchakataji wa madini ili kulinda afya za binadamu, mazingira na kuongeza tija katika sekta ya madini.

Wito huo umetolewa na Kaimu Meneja Ofisi ya Kanda ya Kusini, Hosea Hosea wakati wa Maonesho ya Madini yaliyofanyika wilayani Ruangwa, Mkoa wa Lindi kuanzia Septemba 16 hadi 19, ambapo wadau mbalimbali wa sekta ya madini walipata fursa ya kuelimishwa kuhusu usalama wa kemikali na namna ya kutumia rasilimali za madini kama kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi.

Aidha, Hosea ameeleza kuwa pamoja na madini kuwa chanzo muhimu cha ajira na kipato kwa wananchi na taifa kwa ujumla, matumizi ya kemikali katika shughuli za uchimbaji yanahitaji umakini mkubwa kutokana na athari zinazoweza kujitokeza iwapo kemikali hizo hazitasimamiwa, kuhifadhiwa, kusafirishwa na kutumika kwa kuzingatia taratibu za usalama.

“Kupitia maonesho hayo, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wachimbaji na wadau wengine kuhusu umuhimu wa kufahamu aina ya kemikali wanazotumia, madhara yanayoweza kusababishwa na kemikali hizo pamoja na matumizi sahihi ya vifaa kinga wakati wa kufanya shughuli zinazohusisha kemikali.

Nitoe wito kwa wadau wa kemikali kuhakikisha maeneo yao ya kazi yanakuwa salama kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuhifadhi kemikali, kuzuia kemikali kuvuja au kutapakaa katika mazingira na kuhakikisha mabaki ya kemikali yanashughulikiwa kwa njia salama na kuzingatia matumizi ya vifaa kinga kama vile mavazi maalumu ya kujikinga, glavu, miwani na vifaa vingine vinavyohitajika kulingana na aina ya kemikali kwani ni sehemu muhimu ya usalama wa mfanyakazi na havipaswi kuchukuliwa kama jambo la hiari”, alisema Hosea.

Katika hatua nyingine, Afisa Mahusiano kutoka kampuni ya Lindi Jumbo, Paulo Shauri amepongeza uhusiano mzuri uliopo kati ya wadau wa kemikali na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, akieleza kuwa ushirikiano huo umechangia kuongeza uelewa kuhusu matumizi salama ya kemikali kwani Mamlaka imekuwa karibu na wadau, kuwapa elimu, ushauri na ufuatiliaji wa matumizi salama ya kemikali.

“Uhusiano wetu na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ni mzuri sana. Tumekuwa tukipata elimu na ushauri wa mara kwa mara kuhusu matumizi salama ya kemikali, jambo ambalo limetusaidia kutekeleza shughuli zetu kwa kuzingatia usalama,” alisema Paulo.

Kwa kuzingatia kaulimbiu ya maonesho hayo ya “Madini na Teknolojia, Fursa ya Kiuchumi Lindi,” wadau walihamasishwa kuona teknolojia na usalama kama nyenzo zinazokwenda pamoja katika kuhakikisha utajiri wa madini wa Mkoa wa Lindi unatumika kuongeza fursa za kiuchumi huku ukilinda kizazi cha sasa na kijacho.