TEKNOLOJIA YA DNA YAIPA TANZANIA NGUVU MPYA DHIDI YA UHALIFU
Serikali imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu kwa kuwekeza katika teknolojia za kisasa za uchunguzi wa kisayansi, ikiwemo teknolojia ya vinasaba (DNA), inayosaidia kubaini wahalifu kwa usahihi na kuharakisha utoaji wa haki.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), David Elias, wakati akitoa elimu kwa wananchi katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Alisema serikali imewekeza katika mitambo ya kisasa na mifumo ya kidijitali inayowezesha vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia mwenendo wa sampuli za uchunguzi tangu zinaposajiliwa hadi matokeo yanapotolewa.
"Tunatumia teknolojia ya Vinasaba kuhakikisha mhalifu anayebainika hawezi kuukwepa mkono wa sheria. Lengo ni kujenga Tanzania yenye amani na usalama kwa wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji," alisema Elias.
Alifafanua kuwa pamoja na kusaidia uchunguzi wa makosa ya jinai, teknolojia ya DNA hutumika pia kulinda maliasili za nchi kwa kutambua asili ya nyara za Serikali na kusaidia kudhibiti biashara haramu ya wanyamapori.
Aidha, alisema maabara za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali zina ithibati ya kimataifa, hivyo matokeo ya uchunguzi wa vinasaba yanatambulika kitaifa na kimataifa, jambo linaloongeza uaminifu katika mifumo ya haki na usalama.
Elias alisema uwekezaji huo wa kisayansi unalenga kuifanya Tanzania kuwa mahali salama pa kuishi na mahali salama pa kufanya biashara na kuwekeza.
Hata hivyo, mmoja wa wananchi waliotembelea banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ally Mfaume kutoka Wakala wa Mbegu za Kilimo, alisema elimu aliyopata kuhusu uchunguzi wa vinasaba imemjengea uelewa na kuondoa dhana potofu alizokuwa akizisikia kuhusu huduma hiyo.
Alisema ameelewa kuwa uchunguzi wa DNA ni mchakato wa kisayansi unaotoa majibu sahihi na ya kuaminika, tofauti na baadhi ya taarifa zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii zinazodai kuwa huduma hiyo haina uwazi au hutoa matokeo yasiyo ya uhakika.
Mfaume aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutembelea banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kupata elimu kuhusu uchunguzi wa vinasaba pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na mamlaka hiyo, ikiwemo usimamizi salama wa kemikali. Aidha, aliwapongeza maafisa wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa namna wanavyotoa huduma kwa weledi, uwazi na ukarimu, jambo linalowarahisishia wananchi kuelewa majukumu ya Mamlaka hiyo.