Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

KEMIKALI SALAMA, TAIFA SALAMA: GCLA YATOA ELIMU SABASABA

Imewekwa: 07 Jul, 2026
KEMIKALI SALAMA, TAIFA SALAMA: GCLA YATOA ELIMU SABASABA

Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usimamizi salama wa kemikali na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.

Akizungumza katika banda la GCLA lililopo katika Hema la Jakaya Kikwete namba 36, 37 na 38, Mkurugenzi wa Huduma za Sayansi Jinai, David Elias, alisema wananchi wanaotembelea banda hilo wanapata fursa ya kujifunza kuhusu majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, hususan usimamizi wa kemikali zinazoingia na kutoka nchini.

Alieleza kuwa kemikali zote zinazotumika majumbani, viwandani na katika shughuli mbalimbali za biashara zinapaswa kusajiliwa na Mkemia Mkuu wa Serikali kabla ya kuingizwa nchini ili kuhakikisha zinakuwa salama kwa matumizi yaliyokusudiwa.

"Usajili wa kemikali sasa unafanyika kidijitali. Mwananchi anaweza kufanya usajili akiwa popote kupitia mfumo wa mtandao, na hapa Sabasaba pia tunatoa huduma za usajili na vibali vya kemikali kwa waagizaji na wafanyabiashara," alisema Elias.

Aliongeza kuwa mfumo huo wa kidijitali umeboresha utoaji wa huduma kwa kupunguza muda wa usajili na kurahisisha upatikanaji wa vibali, hatua inayochochea mazingira bora ya biashara na uwekezaji.

Aidha, alisema lengo la GCLA ni kuhakikisha kemikali zote zinazoingia nchini zinakidhi viwango vya ubora na usalama ili kulinda afya za wananchi, mazingira na kukuza uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake, Benadeta Ndemanga, Mjasiriamali kutoka Masasi mkoani Mtwara, alisema amefaidika na elimu aliyopata katika banda la GCLA kuhusu matumizi salama ya kemikali, ambayo itamsaidia kuboresha usalama katika shughuli zake za uzalishaji wa batiki.

Alisema kabla ya kutembelea banda hilo alikuwa akitumia kemikali katika utengenezaji wa batiki bila kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu matumizi yake salama, lakini elimu aliyoipata itamsaidia kujilinda yeye mwenyewe pamoja na wenzake anaofanya nao kazi.

"Nimejifunza mambo mengi kuhusu matumizi salama ya kemikali. Elimu hii itanisaidia kulinda afya yangu, wenzangu tunaofanya kazi pamoja na mazingira yanayotuzunguka. Nawahamasisha wajasiriamali wote wanaotumia kemikali kufika katika banda la Mkemia Mkuu wa Serikali ili wapate elimu hii muhimu," alisema Benadeta.

Elias amewakaribisha wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani kutembelea banda la GCLA kupata elimu kuhusu usimamizi wa kemikali pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na taasisi hiyo katika Maonesho ya Sabasaba.