TANZANIA YANG’ARA AFRIKA KWA TEKNOLOJIA YA VINASABA
Wadau mbalimbali walioshiriki katika kilele cha siku ya maadhimisho ya Vinasaba wameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa juhudi zake katika kusimamia na kuendeleza matumizi ya teknolojia ya vinasaba (DNA) nchini, wakieleza kuwa hatua hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sekta ya afya, uchunguzi wa kisayansi na haki jinai.
Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika tarehe 23 na 24 Aprili 2026, katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Jijini Dodoma, Afisa Tehama, kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Hussen Pashua, ameipongeza Mamlaka hiyo kwa namna inavyoendelea kuimarisha huduma za maabara na matumizi ya teknolojia ya vinasaba.
“Ninapongeza kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka katika kuhakikisha teknolojia ya vinasaba inatumika kwa ufanisi. Hii ina mchango mkubwa katika kuboresha huduma za afya na uchunguzi wa kisayansi,” alisema Pashua.
Naye Mtaalamu wa Teknolojia za Maabara kutoka kampuni ya Thermo Fisher Scientific, Shedrack Masese, ameipongeza Tanzania kwa hatua yake ya kutumia mitambo ya kisasa katika uchunguzi wa vinasaba, akieleza kuwa hatua hiyo inaifanya nchi kuwa miongoni mwa mataifa yanayoongoza barani Afrika katika matumizi ya teknolojia za kisasa za maabara, amesema kuwa matumizi ya teknolojia hizo yanaongeza usahihi na kasi katika uchunguuzi wa sampuli za vinasaba.
“Tanzania imeamua kuwekeza kwenye ubora wa uchunguzi wa kisayansi, Leo hii tunaona mabadiliko makubwa katika kasi ya upatikanaji wa majibu na kiwango cha uaminifu wa matokeo, jambo linaloipa nchi nafasi ya kujipambanua katika sekta ya vinasaba barani Afrika,” alisema Masese.
Kwa upande wake, Mdau kutoka SCIEX Limited, Malik Utenga, ameishauri Mamlaka kuongeza juhudi katika kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya teknolojia ya vinasaba. Amesisitiza kuwa pamoja na uwepo wa teknolojia hizo, bado kuna haja ya kuongeza uelewa kwa jamii ili kuhakikisha zinatumika kikamilifu na kuleta matokeo chanya.
Ameeleza kuwa changamoto kubwa iliyopo siyo tu upatikanaji wa teknolojia, bali ni kiwango cha uelewa wa watumiaji na wadau juu ya umuhimu wake, akibainisha kuwa bila uhamasishaji wa kutosha, hata teknolojia bora inaweza kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Ni muhimu kuongeza uelewa wa jamii kuhusu teknolojia ya Vinasaba na faida zake, ili wananchi waweze kuitumia na kuamini matokeo yake,” aliongeza Utenga.