Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WASIMAMIZI WA KEMIKALI WASISITIZWA UADILIFU

Imewekwa: 21 May, 2026
WASIMAMIZI WA KEMIKALI WASISITIZWA UADILIFU

Wasimamizi wa Kemikali wamehimizwa kutofanya kazi kwa mazoea bila kutumia vifaa kinga wakati wa uzalishaji kwa kutumia kemikali ili kujikinga, kulinda afya zao pamoja na mazingira.

Akizungumza wakati akifunga mafunzo kwa wasimamizi wa kemikali, Mei 19, 2026 mkoani Mwanza, Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Kanda ya Ziwa, John Wanjala, ametoa wito huo kufuatia kuongezeka kwa hatari zinazotokana na matumizi yasiyo salama ya kemikali katika maeneo mbalimbali ya kazi ikiwemo viwandani, maabara, uchimbaji wa madini, hospitali na kwenye shughuli za kilimo.

Meneja alisema kuwa, wafanyakazi wengi wamekuwa wakipuuzia matumizi ya vifaa kinga kama glovu, miwani maalumu, barakoa na mavazi ya kujikinga kwa kisingizio cha uzoefu wa muda mrefu kazini jambo ambalo linaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya yakiwemo matatizo ya mfumo wa upumuaji, ngozi na macho.

“Kemikali nyingi zina madhara ya muda mfupi na ya muda mrefu ambayo huweza kujitokeza baada ya miaka kadhaa, hivyo ni muhimu kufuata taratibu zote za kiusalama kila wakati. Matumizi sahihi ya vifaa kinga ni wajibu wa kila mfanyakazi kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama,” alisema Wanjala.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa semina hiyo walikiri kuwa kuna wafanyakazi wanaofanya kazi bila vifaa kinga kutokana na uzembe au ukosefu wa vifaa hivyo katika maeneo yao ya kazi hivyo, wameiomba Mamlaka na waajiri kuongeza utoaji wa elimu ya usimamizi na utumiaji salama wa kemikali na waajiri kuhakikisha vifaa vinapatikana kwa wakati na kusisitiza kuwa usalama kazini ni jukumu la kila mmoja na si suala la mazoea au uzoefu.