Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MAMLAKA YAKABIDHIWA TUZO YA UTOAJI HUDUMA BORA

Imewekwa: 20 May, 2026
MAMLAKA YAKABIDHIWA TUZO YA UTOAJI HUDUMA BORA

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imetunukiwa tuzo ya Ubora ya Afrika Mashariki kwa kutambua na kuthamini mchango wake wa utoaji huduma bora kwa jamii.

Tuzo hiyo imetolewa na Wizara ya Viwanda kwa niaba ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushindanisha Taasisi mbalimbali zikiwemo za Umma, Sekta za Uzalishaji, Bidhaa za Viwandani na wajasiliamali.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora na Usimamizi wa Vihatarishi, Benny Mallya, amesema Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeibuka mshindi wa kwanza kwa Tanzania na Mshindi wa pili kwa Afrika Mashariki katika sekta ya Umma katika utoaji wa huduma bora na kwamba imeweza kukamilisha ithibati mbalimbali za Maaabara saba ikiwemo Ithibati ya Mifumo ya Ubora.

“Jumuiya ya Afrika ya Mashariki imeweza kutambua, kuona na kuthamini huduma tunazozitoa tunazingatia ubora na mifumo ya utendaji katika Mamlaka lakini pia huduma zetu zote zinazingatia utoaji huduma kwa wakati na kuwasikiliza wadau wetu, hivyo, wameweza kutambua hilo na kuwa sisi ndio washindi wa kwanza pekee tuliotoka Tanzania na Kwenda kupata tuzo hiyo Nairobi nchini Kenya” alisema Mallya.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa mwezi Novemba, 2025 jijini Nairobi nchini Kenya na Sekretarieti ya Afrika Mashariki na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ilikabidhiwa tuzo hiyo hapa nchini na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa sababu haikuweza kuhudhuria mwaka huo 2025.

Akikabidhiwa tuzo hizo katika Ofisi ndogo za Mamlaka Mei 8, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amesema amepokea tuzo hiyo kwa bashasha kubwa na hasa wameipokea tuzo hiyo wakiwa katika kikao cha mwaka cha kupitia mifumo ya ubora ya Menejimenti ya Mamlaka.

“Tuzo hii kwetu ni muhimu sana pamoja na tuzo nyingine ambazo zimekuwa zikitolewa, imefika wakati muafaka kwa sababu sio tuzo ilitolewa tu kama zawadi kuna vigezo vilivyofuatwa, kuna madodoso tuliyoyajaza ya wenzetu na vigezo hivi vimepimwa na watu wengine au Taasisi zilizojaza lakini hatimae tukaibuka washindi katika Sekta ya Umma. Kwa Tanzania tukiwa ni wa kwanza lakini kwa Afrika Mashariki sisi tukiwa ni wa pili. Tuzo hii inatupa moyo wa kuendelea kujituma lakini kutekeleza majukumu yetu kwa kufuata viwango vya Kitaifa na kimataifa lakini kubwa zaidi kutoa huduma zote tunazozitoa kwa wadau na wananchi tuzitoe kwa kiwango kinachostahili na hatimaye mwananchi aone GCLA ni Taasisi bora na aendelee kuiamini kama ambavyo amekuwa akiiamini” alisema Dkt. Mafumiko.