Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

GCLA YASISITIZA UDHIBITI WA KEMIKALI HATARISHI

Imewekwa: 08 Jun, 2026
GCLA YASISITIZA UDHIBITI WA KEMIKALI HATARISHI

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa kemikali za viwandani na majumbani ili kulinda afya za wananchi na mazingira dhidi ya matumizi mabaya ya kemikali hatarishi.

Akifungua Mkutano wa Mwaka wa Wakaguzi wa Kemikali na Maabara za kemia uliofanyika katika Hoteli ya Corridor Springs Arusha, Juni 6, 2026, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, alisema kuwa kupitia Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani, Serikali imeikabidhi Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali jukumu la kusimamia mnyororo mzima wa kemikali pamoja na kemikali bashirifu zinazoweza kutumika kinyume na matumizi stahiki ya kemikali hizo.

Alisema wakaguzi ndio nguzo muhimu katika kuhakikisha kemikali hizo zinadhibitiwa ipasavyo kupitia ukaguzi, usajili, uchukuaji wa sampuli na ukaguzi wa maabara.

“Wakaguzi ndio mliopo mstari wa mbele katika kulinda afya ya jamii, mazingira na wananchi kwa ujumla dhidi ya matumizi yasiyo sahihi ya kemikali hatarishi,” alisema Dkt. Mafumiko.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kujiepusha na rushwa, lugha zisizofaa kwa wadau na ucheleweshaji wa huduma.

Kwa upande wake, mwakilishi wa wakaguzi wa kemikali, Melk Mgonga, aliwahimiza wakaguzi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii, uadilifu na kuzingatia sheria ili kuhakikisha maazimio yote yatakayofikiwa katika mkutano huo yanatekelezwa kikamilifu.

"Twendeni tukatekeleze majukumu yetu kwa weledi na uzalendo, tuimarishe shughuli za ukaguzi kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, na tuhakikishe kuwa maazimio yote yatakayopitishwa katika mkutano huu yanatekelezwa kwa ufanisi kwa manufaa ya taasisi na Taifa kwa ujumla," alisema Mgonga.

Mkutano huo wa siku mbili unatarajiwa kujadili mikakati ya kuboresha utekelezaji wa majukumu ya ukaguzi na usajili wa kemikali pamoja na maabara za kemia nchini.