Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

TANZANIA IPO TAYARI KUKABILIANA NA MAAFA YA KIKEMIKALI NA KIMIONZI

Imewekwa: 16 Mar, 2024
TANZANIA IPO TAYARI KUKABILIANA NA MAAFA YA KIKEMIKALI NA KIMIONZI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali kwa sasa ipo tayari kuhakikisha usalama wa nchi dhidi ya majanga, maafa na dharura mbalimbali zikiwemo za kikemikali, kibaiolojia, kimionzi na kinyuklia.

Mhe. Kassim Majaliwa, alitoa kauli hiyo Machi 14, 2024 wakati wa ufungaji wa mafunzo ya zoezi la utayari dhidi ya dharura za kikemikali na kimionzi Tanzania yaliyofanyika katika viwanja vya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji bandarini jijini Dar es Salaam.

Aidha, Waziri Mkuu amezitaka wizara na taasisi zote zinazohusika na kutekeleza mipango hiyo kuitumia kikamilifu na zitoe ushirikiano kwa wote wanaohitaji kutekeleza miongozo hiyo na pia kukamilisha maandalizi ya nyaraka mbili muhimu za Mpango wa Kitaifa wa Maafa ya Kikemikali, Kibaiolojia, Kiradiolojia na Kinyukilia (CBRN National Action Plan), na Mpango wa Kuitikia wakati wa Dharura za Kinyuklia na Kiradiolojia (Radiological and Nuclear Response Plan) ambazo alizizindua katika hafla hiyo.

“Kupitia nyaraka hizi, mmeweka mikakati ya pamoja ya kitaifa ya namna ya kukabiliana na kujikinga na majanga yatokanayo na dharura za kikemikali, kibaiolojia, kimionzi na kinyuklia. Hivyo nimefurahi sana kusikia nyaraka hizo zimezingatia masuala muhimu ya kisera, uzoefu wa kukabiliana na majanga kitaifa na kimataifa pamoja na matakwa ya kisheria na itifaki za kimataifa,” alisema Mhe. Majaliwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu, Profesa Lazaro Busagala alisema kuwa umuhimu wa zoezi hilo ni kuhakikisha kwamba inapotokea dharura ya kibaiolojia, kikemikali na kimionzi, timu ya wataalam inahakikisha kuwa usalama unakuwepo na pia kuokoa maisha ya watu pamoja na mali.

Naye, Mkemia Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amesema kuwa mazoezi ya utayari dhidi ya dharura za kikemikali na kimionzi yataendelea kufanyika mara kwa mara kwa lengo la kujenga utayari wa timu ya Taifa ya kujiandaa na kukabiliana na dharura za kitaifa.