NPS YASISITIZA USHAHIDI WA KISAYANSI KESI ZA JINAI
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Tabora, Chema Maswi, amezitaka vyombo vya uchunguzi kupeleka majalada yenye ushahidi wa Kisayansi kwani ushahidi huo unaaminika zaidi na Mamlaka za utoaji Haki duniani.
Maswi amesema hayo Oktoba 9, 2026 wakati akifungua mafunzo ya Sayansi Jinai kwa wadau wa Haki Jinai yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma mkoani Tabora.
“Dunia imebadilika sana uchunguzi wa Kisayansi unaaminika sana na Mahakama duniani kote, kwa hiyo tunataka kutoka kwenye zama za kutegemea nani alisema, nani alikiri badala yake Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inapendelea kuona majalada mnayotuletea yawe na ushahidi wa Kisayansi” alisema Maswi.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Tabora, Mbaruku S. Mbaruku ameishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa mafunzo hayo huku akiwataka washiriki kuwapa mafunzo hayo wachunguzi wengine ambao hawajabahatika kushiriki mafunzo hayo.
“Tunaishukuru sana GCLA, tutafanyia kazi na nawataka wapiganaji wenzangu hii elimu tusibaki nayo wenyewe tukirudi ofisini tuwafundishe wenzetu ili kuboresha utendaji wa ofisi zetu” alisema Mbaruku.
Aidha Meneja wa Maabara ya Sayansi Jinai Baiolojia na Vinasaba, Dkt. Fidelis Bugoye amesema mafunzo hayo yamekuwa ya vitendo zaidi ili kubaini kama kuna mapungufu katika utendaji ili kuboresha na kuisaidia GCLA kupata sampuli zenye ubora na umahiri ili kurahisisha mchakato wa uchunguzi.
“Tumefanya mafunzo haya kwa vitendo zaidi ili kubaini kama kuna mapungufu mbalimbali kwenye utendaji ili sisi wataalamu tujue namna ya kuwasaidia ili wawe bora ili GCLA ipate sampuli zenye umahiri ili kurahisisha mchakato wa uchunguzi” alisema Dkt. Bugoye.
Theraiya Buriani na Salumu wamesema mafunzo hayo yatawasaidia katika utekelezaji wao wa majukumu huku wakiiomba GCLA kuendelea kuwapa mafunzo hayo kwa vitendo mara kwa mara.
“Tunaishukuru GCLA kwa mafunzo haya mazuri sana ya vitendo ambayo yatatusaidia sana na tunaomba yawe mara kwa mara ili kutupa uzoefu kwa vitendo kama leo” walisema wapelelezi hao.