GCLA YANG’ARA MAONESHO MADINI GEITA
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imeibuka miongoni mwa taasisi zilizofanya vizuri katika Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini 2026, baada ya kutwaa tuzo tatu katika makundi mbalimbali ya washiriki wa maonesho hayo yaliyofanyika mkoani Geita.
GCLA imeshinda nafasi ya pili katika tuzo kwa Taasisi Wezeshi za Serikali katika Sekta ya Madini, nafasi ya tatu katika kundi la Taasisi za Umma, pamoja na tuzo ya Maalum ya Mdhamini wa Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini 2026.
Tuzo hizo zilitolewa Oktoba 2, 2026 katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa EPZ Bombambili, Geita, na kukabidhiwa na Mgeni Rasmi, Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Dkt. Latifa Mohammed Khamis.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Khamis aliwataka washiriki, hususan wanawake wanaojishughulisha na biashara, kutumia maonesho hayo kama fursa ya kujifunza, kuboresha shughuli zao na kujiandaa kwa fursa zijazo.
“Maonesho haya tuyatumie kama darasa la kujifunza. Hususan wanawake, mnapaswa kutumia uzoefu na ujuzi mlioupata hapa kama ngazi ya kuboresha shughuli zenu na kufanya vizuri zaidi katika maonesho yajayo,” alisema Dkt. Khamis.
Alisema ushiriki katika maonesho unapaswa kwenda sambamba na kujifunza, kubadilishana uzoefu na kutumia fursa zinazopatikana ili kuongeza ufanisi katika shughuli za uzalishaji na biashara.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda ya Ziwa, John Wanjala, alisema mafanikio hayo ni matokeo ya maandalizi mazuri na ushirikiano wa pamoja wa watumishi wa Mamlaka katika maonesho hayo.
“Tuzo hizi ni heshima kubwa kwa GCLA na zimetupa motisha ya kuendelea kuboresha huduma, kuongeza ubunifu na kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini kama mdau muhimu,” alisema Wanjala.
Wanjala aliongeza kuwa maonesho ya mwaka huu yamekuwa na tija na ushindani mkubwa, huku yakitoa fursa kwa GCLA kuwafikia wananchi na wadau wa sekta ya madini na kuwapatia elimu kuhusu huduma na majukumu ya Mamlaka.
Katika maonesho hayo, GCLA imetoa elimu kuhusu matumizi salama ya kemikali, hususan kwa wachimbaji wakubwa na wadogo wa madini, pamoja na huduma za uchunguzi wa sampuli za jinai na uchunguzi wa ubora na usalama wa bidhaa na dawa asili kwa matumizi ya binadamu.
Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini 2026 yamefanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili, Geita, kuanzia Septemba 23 hadi Oktoba 3, 2026, yakishirikisha taasisi za umma, kampuni binafsi na wadau mbalimbali wa sekta ya madini. Maonesho hayo yamefungwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Maonesho hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu “Madini ni Utajiri – Tuwajibike kwa Pamoja Kufikia Dira ya Taifa 2050.”