USALAMA WA NGUVU KAZI UPEWE KIPAUMBELE KWENYE UCHIMBAJI
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Mwigulu Nchemba (MB) amewataka wadau wa Sekta ya Madini kuzingatia usalama wa nguvu kazi ili faida inayopatika kwenye shughuli za uchimbaji iweze kuwanufaisha watanzania.
Dkt. Nchemba amesema hayo Oktoba 3, 2026 wakati akifunga maonesho ya tisa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Mkoa Geita.
“Nawapongeza wadau wa madini kwa kufanikisha maonesho ya Geita, Mafanikio ya sekta ya madini yanahitaji kila mdau kutekeleza wajibu wake kwa kushirikiana ili kupata matokeo chanya, rasilimali watu inapaswa kulindwa kwa kuzingatia miongozo yote ya shughuli za uchimbaji wa madini ikiwemo kuchunguza afya mara kwa mara na usalama kazini” alisema Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde, akisisitiza kuwa madini ni Sayansi hivyo wachimbaji hawana budi kuzingatia uchunguzi wa kisayansi ili kuongeza tija
“Sekta ya madini inachangia asilimia 10.3 ya pato la Taifa huku wachimbaji wadogo wakichangia 40% ya asilimia 10.3 ya sekta nzima, na niwaambie Madini ni Sayansi madini yanaongozwa kwa utafiti, asilimia 10 ya pato la sekta ya madini inawekwa kwenye utafiti ili kuleta Tija kwenye sekta hii” alisema Waziri Mavunde
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti amewataka wadau wa uchimbaji kuimarisha usalama wa wachimbaji ili kuongeza tija ya maendeleo ya sekta ya madini ikiwemo matumizi salama ya Kemikali pamoja na matumizi ya vifaa Kinga.
“Lengo la maonesho haya ni kutoa elimu juu ya mbinu za uchenjuaji na uchimbaji wa madini na kuhamasisha wachimbaji wadogo na kati kutangaza fursa zilizopo katika sekta ya madini, niwatake wadau wote kuimarisha usalama wa wachimbaji ili kuongeza tija ya maendeleo ya sekta ya madini” alisema Mnyeti.
Baadhi ya Wachimbaji wadogo wameishukuru Serikali kwa kutenga asilimia 10 ya pato linalotoka kwenye sekta ya madini kutumika kwenye utafiti utakaoongeza tija ya uchimbaji.
“Kiukweli asilimia hizi 10 zinatutoa kwenye maisha ya kubeti tunaanza kuchimba tukiwa na uhakika kuwa madini yapo ama hayapo” walisema Joseph Malaki na Meri John.