Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MKEMIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA WATUMISHI KUMPA USHIRIKIANO MENEJA

Imewekwa: 11 Nov, 2026
MKEMIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA WATUMISHI KUMPA USHIRIKIANO MENEJA

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewataka watumishi wa Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kumpa ushirikiano Meneja wa mpya wa Kanda ili kuweza kutimiza malengo ya Kanda na Mamlaka kwa ujumla.

Mkemia Mkuu wa Serikali amesema hayo Oktoba 26, 2026 jijini Mbeya wakati akimtambulisha rasmi Meneja mpya wa Ofisi ya Kanda, Everlight Matinga, kwa watumishi wa Kanda hiyo.

“Huyu ndio Meneja na majukumu yote anapaswa kufanya kama Meneja wa kanda.

Dawati la usajili na ukaguzi ndio wasaidizi wakubwa wa meneja katika masuala ya utekelezaji wa sheria ya kemikali katika usajili na ukaguzi wa wadau pamoja na Dawati la usimamizi wa maabara katika masuala yote yanayohusu uchunguzi wa kimaabara.  Tunapaswa kumsaidia meneja ili kuwezesha majukumu ya Kanda kutekelezeka na tusijenge makundi ila tunapaswa kuwa kitu kimoja ili kuwezesha Kanda kuweza kutimiza malengo iliyojiwekea kwa mwaka wa fedha 2026-2027 pamoja na malengo ya Mamlaka kwa ujumla” alisema Dkt. Mafumiko.

Aidha, aliwataka watumishi kujenga umoja na mshikamano na kuwa na utaratibu wa kuwa na vikao vya mara kwa mara vitakavyowawezesha kujadili mambo yao ya kazi kwa kina na kutatua changamoto wanazokutana nazo wakati wanapokuwa wanatekeleza majukumu ya kazi.

Naye Kaimu Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Everlight Matinga, amemshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kumuamini na kumteua kuongoza Kanda hiyo na anaamini atailinda imani hiyo kwa kutekeleza majukumu yake kwa nguvu na ufanisi mkubwa kwa kushirikiana na watumishi wenzake wa Kanda.

“Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwako kwa imani kubwa uliyonipa ya kuona nastahili kukusaidia majukumu katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, pia nashukuru kwa yote yaliyosemwa. Napenda kuwashukuru watumishi wa Kanda kwa kumuaga mtangulizi wangu na kunikaribisha. Naahidi kushirikiana na na wadau wetu wote pamoja na Kanda nyingine pia katika masuala mbalimbali ya kiutnedaji ikiwemo mafunzo kwa wadau wetu.

Binafsi huwa naamini katika K tatu ambazo ni kupendana, kushirikiana na kuwajibika vizuri Ili kuweza kutimiza malengo yetu. Tunakuahidi Mkemia Mkuu wa Serikali kwamba tutashirikiana kwa pamoja ili kutimiza malengo yetu kama Kanda. Kila kada ni muhimu ndani ya kanda hivyo tunahitajika kushirikiana ili kuweza kufikia malengo yetu” alimaliza Kaimu Meneja.