BARAZA LAPOKEA TUZO ZA USHINDI WA MAONESHO YA MADINI
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeibuka na ushindi wa tuzo tatu katika Maonyesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika mkoani Geita na kuhitimishwa Oktoba 3, 2026, Tuzo hizo zimekabidhiwa rasmi kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka, Dkt. Fidelice Mafumiko, katika Kikao cha Nne cha Baraza la Nane la Wafanyakazi wa Mamlaka, kilichofanyika katika Hoteli ya Cate, mkoani Morogoro, Oktoba 9, 2026.
Akikabidhi tuzo hizo, Meneja wa Kanda ya Ziwa, John Faustine Wanjala, amemshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuiwezesha Mamlaka kushiriki katika maonesho mbalimbali, ikiwemo Maonesho ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika mkoani Geita, ambako imefanikiwa kushinda tuzo tatu kutokana na utendaji wake.
Wanjala alisema tuzo hizo ni ushahidi wa juhudi zinazofanywa na Mamlaka katika kutekeleza majukumu yake na kutoa huduma bora kwa wananchi, huku akibainisha kuwa mafanikio hayo yanaonesha nafasi muhimu ya taasisi hiyo katika sekta ya madini.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzikabidhi tuzo hizi mbele ya Baraza lako ili watumishi na wajumbe wengine waweze kuona jitihada zinazofanywa na Mamlaka. Mbali na kutekeleza majukumu yetu kwa kiwango cha asilimia kubwa, mafanikio haya yanaonesha nafasi kubwa tuliyonayo nchini katika kutoa huduma, Pia, tumeshika nafasi ya pili kama wadau wa uwezeshaji katika sekta ya madini,” alisema Wanjala.
Kwa upande wake, Mkemia Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Baraza, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewapongeza watumishi wote walioshiriki kuiwakilisha Mamlaka katika maonesho hayo na kuwataka kudumisha juhudi hizo ili kuhakikisha taasisi inaendelea kupata tuzo katika maonesho mbalimbali kila mwaka.
“Tunawapongeza sana kwa kazi nzuri najua ukiwa Mkuu wa Taasisi unakuwa na vyanzo vya habari ambavyo unakuwa unafuatilia utendaji unakwendaje, kuna wakati tulionekana wakali sana viongozi na wakati mwingine kuna watu walipoteza sauti na muda mwingine nilienda kuhamasisha kwamba twende kwa njia hii, juhudi zote hizo ndo zilizozaa hizi tuzo,” Alisema Dkt. Mafumiko.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Shadrack Mkodo, amempongeza Dkt. Mafumiko kwa kuliongoza Baraza kwa viwango vya juu na kupendekeza kuwepo kwa mafunzo maalumu kwa wajumbe ili kuwaongezea ujuzi katika uongozi na utumishi wa umma, kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu yao kwa ubora na ufanisi.
“Ninakumbuka Baraza la mwisho nililoshiriki maeneo mengine, niliwaambia, mkipata nafasi, wapelekeni watu wakajifunze kwenye Baraza la GCLA, maana hili ni Baraza la viwango. Kama yapo mabaraza manne au matano katika nchi hii yanayofanya vizuri, Baraza la GCLA ni mojawapo,” alisema.Mkodo.