Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MASHARIKI WAPONGEZWA KWA KUFIKIA MALENGO YA MWAKA 2025/2026

Imewekwa: 17 Aug, 2026
MASHARIKI WAPONGEZWA KWA KUFIKIA MALENGO YA MWAKA 2025/2026

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewapongeza watumishi wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda ya Mashariki kwa kuweza kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Mkemia Mkuu wa Serikali ametoa pongezi hizo Agosti 15, 2026 wakati wa kikao cha pamoja na watumishi wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki kilichofanyika katika Ofisi za Kanda jijini Dar es Salaam.

“Napenda kuwapongeza kwa kumaliza mwaka wa fedha 2025/2026 kwa mafanikio makubwa ya kutimiza malengo mliyojiwekea ikiwemo kufikia lengo la ukusanyaji wa mapato ambalo mlijiwekea. Katika hili Kanda ya Mashariki mmetubeba na nawapongeza sana wote, kwa sababu kila mmoja wenu ana mchango katika kutimiza lengo hili la ukusanyaji wa mapato ya Serikali. kila mmoja ajivunie katika hili.” alisema Dkt. Mafumiko.

Mkemia Mkuu wa Serikali amewataka kutoridhika katika mafanikio waliyopata bali kuongeza jitihada zaidi na kuimarisha utendaji kazi na masuala ya nidhamu kwa ujumla kwa kutunza rasilimali za taasisi, kuzingatia Sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma.

Naye Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa, akitoa neno la shukrani alisema anashukuru kwa pongezi na maelekezo yote aliyotoa Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice `Mafumiko, na alichojifunza kutoka kwake ni kufanyia kazi kwa haraka na umakini taarifa zote ambazo zinawasilishwa kwake kwa ajili ya kufanya maamuzi. Aliongeza kwa kusema mshikamano, uwajibikaji, ushirikishwaji, kufanyia kazi maoni ya wadau, kutenda kulingana na wakati na upendo kati yao ndio nguzo kuu ya kutimiza malengo yao kwa ukamilifu ndio maana hata kwa mwaka 2026/2027 wameshakaa na kuweka mikakati ya kutekeleza malengo ya mwaka huo.