Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MAPINDUZI YA VINASABA YACHOCHEA MAENDELEO YA AFYA NA HAKI JINAI TANZANIA

Imewekwa: 29 Apr, 2026
MAPINDUZI YA VINASABA YACHOCHEA MAENDELEO YA AFYA NA HAKI JINAI TANZANIA

Serikali imesema matumizi ya teknolojia ya uchunguzi wa vinasaba yanafungua ukurasa mpya wa fursa kwa maendeleo ya jamii, yakichochea mageuzi katika sekta ya afya, haki jinai, na uhifadhi wa rasilimali za taifa.

Akifungua maadhimisho ya Siku ya Vinasaba Tanzania 2026 yanayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi akimuwakilisha Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema kuwa teknolojia ya vinasaba imekuwa nguzo muhimu katika utoaji wa huduma za afya zenye ubora na viwango vya kimataifa.

“Katika sekta ya afya, teknolojia ya DNA imewezesha mafanikio makubwa ikiwemo utambuzi sahihi wa uhusiano wa kijenetiki katika upandikizaji wa figo na uroto, pamoja na maendeleo ya tiba za kisasa kama tiba jeni na utengenezaji wa chanjo zinazotumia mifumo ya vinasaba” alisema Naibu Waziri wa Afya.

Mbali na afya, Naibu Waziri alisisitiza mchango wa teknolojia ya vinasaba katika sekta ya haki jinai na ujangili, akibainisha kuwa ushahidi wa kisayansi unaotokana na vipimo vya maabara umeongeza ufanisi katika utoaji wa haki mahakamani, kwa kusaidia kubaini wahusika wa uhalifu au kuwaondolea tuhuma wasiohusika.

“Teknolojia hii pia imekuwa msaada mkubwa katika kutambua wahanga wa majanga na hata katika mapambano dhidi ya ujangili, kwa kubaini aina ya mnyama, jinsia na uhusika wa mtuhumiwa,” alisema Dkt.Florence.

Aidha, alisema kuwa Serikali, imeendelea kuwekeza katika miundombinu na vifaa vya kisasa ili kuimarisha uchunguzi wa vinasaba nchini. Miongoni mwa uwekezaji huo ni ujenzi wa maabara ya kisasa yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 16 pamoja na ununuzi wa mitambo ya kisasa ya uchunguzi wa vinasaba.

Kwa upande wake, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, alieleza kuwa teknolojia ya vinasaba imekuwa chachu ya mapinduzi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, mifugo na haki jinai, huku akibainisha kuwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imekuwa ikitumia teknolojia hiyo kwa zaidi ya miaka 20.

Alifafanua kuwa katika kipindi cha Januari 2025 hadi Machi 2026 pekee, jumla ya sampuli 8,956 zilifanyiwa uchunguzi, zikisaidia kutatua masuala mbalimbali ya kijamii na kisheria.

Alibainisha kuwa hadi sasa, maabara nne zimekwishasajiliwa rasmi nchini kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba, huku maombi 29 ya vibali vya utafiti yakishughulikiwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria.

Mkutano huo, unaowakutanisha zaidi ya wataalamu 400 kutoka sekta mbalimbali, umeelezwa kuwa jukwaa muhimu la kujadili mafanikio yaliyofikiwa, changamoto zilizopo pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha matumizi ya teknolojia ya vinasaba nchini.

Maadhimisho hayo yaliyobebwa na kauli mbiu “Kufungua Fursa kwa Jamii kupitia Uchunguzi wa Vinasaba” yamebeba matumaini mapya kwa Tanzania katika kutumia sayansi na teknolojia ya vinasaba kama nyenzo ya kuleta maendeleo endelevu, huku yakisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, ulinzi wa taarifa na uwekezaji endelevu katika rasilimali watu na miundombinu.