Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MADEREVA WANAOSAFIRISHA KEMIKALI WATAKIWA KUZINGATIA MAFUNZO

Imewekwa: 23 Jun, 2026
MADEREVA WANAOSAFIRISHA KEMIKALI WATAKIWA KUZINGATIA MAFUNZO

Msimamizi wa Dawati la Ukaguzi wa Kemikali wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Ofisi ya Kanda ya Kati, Suitbert Sinduhije amesema Mamlaka imedhibiti Kemikali ya Sulphur iliyomwagika eneo la Mikumi na amewataka Madereva kuzingatia mafunzo wanayopata huku akiwasihi Wananchi kutoa taarifa kwa Mamlaka pindi ajali za Kemikali zinapotokea.

Sinduhije amesema hayo Juni 18, 2026 baada ya kukamilisha zoezi la kuiondoa Kemikali iliyomwagika ikiwa inasafirishwa kwa njia ya barabara eneo la Mikumi mkoani Morogoro.

“Tumepata Taarifa kuhusu Kemikali hii iliyomwagika tumefika kwa ajili ya kudhibiti na hali ni shwari athari ndogo ndogo zilizosababishwa na vumbi la Kemikali hiyo ni kusikia muwasho mwilini na usoni ambapo kunywa maji mengi na kuosha eneo lililofikiwa na Kemikali inamuweka mwananchi salama kabisa. Nawasihi Madereva kuzingatia mafunzo ambayo Mkemia Mkuu amewapa, pia nawaomba wananchi waendelee kutupa taarifa pindi matukio haya yanapotokea ili yakabiliwe kwa wakati bila madhara kwa wananchi” alisema Sinduhije

Aggrey Kinzilizi na Yusta Komba ni wakazi wa Mikumi wanaofanya biashara kando ya Barabara wamesema wamesikia muwasho sehemu zao za mwili baada ya vumbi la Kemikali hiyo kuwafikia.

“Magari yanapopita yanatibua ile Kemikali inakuja huku kiukweli ni kuwashwa mwanzo mwisho, Mkemia amefika akatueleza tumeweza kunawa kwa maji mengi kwa sasa hamna tena ule muwasho, tunaomba hawa wanaosafirisha Kemikali wasiwe peke yao Mkemia wa Serikali awe anawafuatilia kwa nyuma ili changamoto hizi zisitukute” walisema wakazi hao wa Mikumi.