HIFADHIDATA YA VINASABA YAZIDI KUPEWA KIPAUMBELE TANZANIA
Wakati dunia ikiendelea kupiga hatua katika matumizi ya sayansi ya vinasaba, wataalam nchini wameelezea umuhimu wa uanzishwaji na ulinzi madhubuti wa hifadhidata ya Vinasaba (DNA) ili kulinda usalama wa taifa na faragha ya wananchi.
Akizungumza katika Kongamano la Siku ya Vinasaba Tanzania, lililofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Dodoma, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kairuki, Prof. Edda Vuhahula, alieleza kuwa hifadhi ya data ya Vinasaba ni nyenzo muhimu inayoweza kusaidia kutambua watu, kufuatilia magonjwa na hata kuunganisha ndugu waliopoteana.
Alisema kuwa endapo taarifa za Vinasaba vya mtu zitahifadhiwa, zinaweza kutumika baadaye kumtambua mtu aliyepata ajali, kufariki bila kutambulika, au hata kusaidia katika uchunguzi wa magonjwa ya kurithi.
“Ni muhimu sana nchi kuwa na hifadhidata ya DNA ya watu wake. Serikali tayari imeanza hatua hizo kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), na mchakato umefikia hatua nzuri,” alisema Profesa Edda.
Hata hivyo, Profesa Edda alionya juu ya hatari inayoweza kujitokeza iwapo data za vinasaba zitaendelea kuchukuliwa na kupelekwa nje ya nchi bila udhibiti madhubuti. Alifafanua kuwa katika baadhi ya matukio, sampuli za wagonjwa hupelekwa nje ya nchi kwa uchunguzi, lakini hakuna uhakika wa nini kinafanyika kwa data hizo baada ya majibu kurejeshwa.
“Hatari yake ni kubwa. Mataifa ya nje yanaweza kupata uelewa wa kina wa Vinasaba vyetu, na hilo linaweza kutumika vibaya, hata kutengeneza madhara ya kiafya kwa vizazi vijavyo,” aliongeza Profesa Edda.
Kwa mujibu wa mtaalam huyo, ingawa Tanzania ina sheria zinazodhibiti matumizi ya Vinasaba, bado kuna changamoto katika usimamizi wake. Alisisitiza kuwa taasisi zote zinazohusika na Vinasaba ikiwemo hospitali, vituo vya utafiti na vyombo vya dola zinapaswa kushirikiana na kufuata sheria kikamilifu.
Aidha, alisisitiza kuwa hakuna taasisi au mtu anayepaswa kufanya uchunguzi wa Vinasaba bila kibali cha serikali kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Pia, alishauri hatua kali zichukuliwe kwa wanaokiuka taratibu, ikiwa ni pamoja na kuchapisha tafiti bila idhini.
Kwa upande wa matumizi ya teknolojia ya DNA nchini, Profesa Edda alibainisha kuwa bado yako chini kutokana na uhaba wa maabara, wataalamu na uelewa mdogo wa wananchi.
Alipendekeza kuongezwa kwa maabara zenye viwango, kuimarisha mafunzo ya wataalamu, pamoja na kutoa elimu kwa umma ili wananchi watambue kuwa Vinasaba (DNA) ni sehemu ya utu wao na inapaswa kulindwa.
“Wananchi waelimishwe kuwa DNA ni utambulisho wao wa msingi. Si jambo la kuruhusu kila mtu kuifahamu au kuitumia bila mipaka,” alisisitiza.
Naye Dkt. Irene Rweikiza, daktari wa binadamu anayesoma Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Bioteknolojia katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Nairobi, amesema hifadhidata ya DNA ina umuhimu mkubwa katika kuimarisha huduma za afya nchini.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukitumia zaidi taarifa za Vinasaba katika kutibu magonjwa, lakini mjadala wa mkutano huu umeonesha wazi umuhimu wa kuwa na kanzidata imara ya Vinasaba, hasa katika uchunguzi wa mapema wa magonjwa, ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kujitokeza baadaye,” alisema Dkt. Irene.