DNA INAVYOFUNGUA FURSA KWA VIJANA
Vijana Nchini wamehimizwa kutumia fursa zinazotokana na sayansi ya vinasaba (DNA) Kujijengea mustakabali kupitia tafiti, ubunifu na Ajira zinazotolewa katika sekta ya Afya na teknolojia.
Akizungumza katika kilele cha siku ya Maadhimisho ya Vinasaba Tanzania, 24 aprili, 2026 yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete Dodoma, Mtafiti kutoka Kilimanjaro Clinical Research Institute (KCRI), Davis Kuchaka, amesema kuwa uelewa na ushiriki wa vijana katika tafiti za Vinasaba umeanza kufungua milango mipya ya mafanikio ambayo awali wengi hawakuifahamu na kuitilia maanani.
‘’DNA imekuwa eneo linalowapa fursa vijana katika kufanya tafiti za kimataifa na hata kujipatia Ajira, kupitia kushiriki miradi ya kisayansi inayolenga kutatua changamoto mbalimbali za kiafya, kwa sababu tunapozungumzia Vinasaba tunaongelea pia ajira za kesho, vijana wakijikita katika eneo hili wanaweza kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto” alisema Kuchaka.
Naye Mdau Kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Dkt. Catherine Gwandu, amesema kuwa uwepo wa maarifa ya Vinasaba yamewafungulia vijana fursa mbalimbali ikiwemo kupata mafunzo ya kitaaluma na kujenga taaluma katika sayansi na teknolojia.
“Kupitia vijana wanaweza kuona sayansi kama eneo la fursa si kwa ajira tu bali pia kwa ubunifu, tafiti na kutengeneza suluhisho kwa changamoto za kijamii, kadri dunia inavyozidi kuwekeza katika vinasaba na teknolojia za afya, ndivyo fursa kwa vijana zinavyozidi kuongezeka kinachohitajika ni wao kujitokeza na kuzitumia fursa,” amesema Gwandu.
Maadhimisho hayo yamelenga kutatua changamoto zinazohusiana na masuala ya vinasaba ikiwemo katika masuala ya haki, utafiti na maendeleo ya jamii ambayo kwa mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo “Kufungua Fursa kwa Jamii kupitia Uchunguzi wa Vinasaba.”