MKEMIA MKUU WA SERIKALI: TAFITI ZETU ZILENGE KUHUDUMIA JAMII
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, ametoa wito kwa watafiti na watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kujikita zaidi katika kufanya tafiti zenye manufaa kwa jamii, hususan zile zinazolenga kulinda afya za binadamu na mazingira.
Akizungumza Novemba 11, 2025, wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Pili ya Utafiti ya Mamlaka uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkemia, jijini Dar es Salaam, Dkt. Mafumiko alisisitiza kuwa tafiti ni nyenzo muhimu katika kuchangia maendeleo ya Taifa na kuboresha maisha ya Watanzania.
“Ni wajibu wetu kufanya tafiti kama ambavyo sheria inatutaka, pamoja na kufuata miongozo ya Serikali ili kuchangia utatuzi wa changamoto zinazoikabili jamii,” alisema Dkt. Mafumiko.
Alieleza kuwa moja ya majukumu makuu ya GCLA ni kufanya tafiti zenye kuleta manufaa kwa jamii, kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Sura ya 177 (Sheria Na. 8 ya mwaka 2016). Pia alikumbusha kuwa utafiti si jambo jipya katika taasisi hiyo, akitolea mfano kuwa ugunduzi wa vimelea vya malaria ulifanyika katika taasisi hiyo, jambo linalodhihirisha mchango wake mkubwa katika historia ya sayansi nchini.
Aidha, Dkt. Mafumiko aliipongeza Kamati ya kwanza ya Utafiti kwa kazi nzuri waliyoifanya, ikiwemo kuandaa taratibu na nyaraka mbalimbali pamoja na kusimamia tafiti zilizochangia kutatua changamoto za kiafya na kimazingira nchini.
Mkemia Mkuu wa Serikali, pia alitoa maagizo mahsusi kwa Kamati mpya kuhakikisha tafiti zote zinazingatia miongozo ya Serikali na kulenga katika kutatua changamoto halisi za jamii na kuandaa maandiko ya tafiti yenye ubora yanayoweza kuvutia ufadhili wa rasilimali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Utafiti, Dkt. Fidelis Bugoye, alimshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuwaamini na kuwateua kushika majukumu hayo. Aliahidi kuwa Kamati itafanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kuleta mageuzi katika utatuzi wa changamoto zinazokabili Mamlaka, Wizara na jamii kwa ujumla.
Aidha, aliwataka wajumbe wenzake kudumisha ushirikiano na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kufanikisha malengo yaliyowekwa na kuacha alama chanya kwa kamati zitakazofuata.