WAKAGUZI WAASWA KUFANYA MAAMUZI KWA KUZINGATIA MAARIFA NA UJUZI
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewataka wakaguzi wapya Kemikali na Maabara za Kemia kutambua wajibu na mamlaka watakayokuwa nayo kwa mujibu wa matakwa ya sheria na kufanya maamuzi kwa kuzingatia maarifa na ujuzi kwenye majukumu yao.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema hayo Novemba 10, 2025 wakati akifungua mafunzo kwa Wakaguzi wapya (39) wa Kemikali na Maabara za Kemia yaliyofanyika katika Ofisi za Kanda ya Mashariki, Dar es Salaam.
“Nawaelekeza mtumie nafasi hii adhimu kuwa wasikivu na wenye utayari wa kujifunza kwa kusikiliza watoa mada na kuuliza maswali kwa lengo la kujenga uelewa zaidi. Kwa kuzingatia maarifa na ujuzi mtakaopata katika mafunzo haya, ni matumaini yangu kuwa mtajenga uelewa na weledi wa kutosha kutekeleza jukumu hili muhimu kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali,” alisema Dkt. Mafumiko.
Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali amesisitiza wakaguzi kuepuka kuwa na changamoto zinazotokana na kukosekana weledi wa mkaguzi hasa katika kujaza dodoso kwa makini wakati wa ukaguzi na kuandika taarifa sahihi na stahiki.
Pia, Dkt. Mafumiko ameongeza kuwa ni takwa la kisheria kwa wakaguzi kupata mafunzo hayo kabla ya kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali na kupewa vitambulisho kwa ajili ya kufanya ukaguzi kwa wadau wanaojishughulisha na kemikali au uchunguzi katika Maabara za Kemia.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo amesema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo wakaguzi wapya pamoja na kukidhi matakwa ya kisheria, na hivyo kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria.