MKEMIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA WAJUMBE WA BARAZA KUWAJIBIKA
Mkemia Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanayakazi la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewataka watumishi wa Mamlaka kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika sehemu zao za kazi ili tija iweze kuonekana katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akazungumza wakati akifungua Kikao cha Pili cha Baraza la Nane la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kilichofanyika Oktoba 23, 2025 katika mkoani Morogoro, Mkemia Mkuu wa Serikali amewakumbusha watumishi wa Mamlaka kuendelea na utamaduni wa kufanya kazi kwa weledi na ufanisi ili kufikia malengo ya taasisi.
“Ni wajibu wa kila mtumishi kufuata misingi ya kazi na endapo mtaamua kutekeleza majukumu yenu kwa kuzingatia weledi, ufanisi na uwajibikaji, ni dhahiri kuwa tija itaonekana kazini,” alisema Dkt. Mafumiko.
Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali amebainisha kuwa jukumu la msingi la Baraza la Wafanyakazi ni kushauri Menejimenti katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu ambayo taasisi inawajibika kwa umma na kujadili bajeti ya taasisi na utekelezaji wake kwa kila mwaka wa fedha. Pia, ametoa rai kwa wajumbe wa Baraza la wafanyakazi la Mamlaka kutumia nafasi ya uwakilishi kwa kutetea na kulinda haki kwa maslahi ya watumishi na taifa kwa ujumla.
“Maamuzi yanayopitishwa ndani ya Baraza hili ni kwa ajili ya maslahi ya taasisi, hivyo, wajumbe tulioko hapa kwa uwakilishi tuendelee kuwahamasisha wenzetu kwa kuwapa mrejesho kutokana na maamuzi tuliyofikia,” aliongeza Mkemia Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE, tawi la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Adam Mbugi, amempongeza Mkemia Mkuu wa Serikali, Bodi pamoja na Menejimenti kwa mahusiano mazuri na Wafanyakazi na ushirikiano wa pamoja hali inayopelekea Baraza kuwa la usikivu na uwazi.
Pia, Mjumbe wa Balaza la Wafanyakazi la Mamlaka, Martha Msola, amepongeza Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka, Dkt. Fidelice Mafumiko, kwa ambavyo amekuwa akiongoza Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka kwa kutoa demokrasia y hali ya juu kwa Wajumbe kuweza kutoa maoni na ushauri.