Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WATUMISHI WAPYA WAASWA KUFUATA UTAMADUNI

Imewekwa: 30 Jul, 2025
WATUMISHI WAPYA WAASWA KUFUATA UTAMADUNI

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewataka watumishi wapya na waliohamia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuhakikisha wanaelewa majukumu ya Mamlaka na utamaduni wake ili iwawezeshe katika utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi.

Dkt. Mafumiko amesema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya awali kwa waajiriwa wapya na watumishi waliohamia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali yaliyofanyika Dar es Salaam Julai 28, 2025.

“Kila taasisi ina majukumu na utamaduni tofauti na taasisi nyingine, hivyo kutokana na sababau hiyo Mamlaka imeweka utaratibu wa kutoa mafunzo ya awali kwa watumishi wote wanaojiunga na Mamlaka kwa njia ya ajira mpya au uhamisho kwa lengo la kuwafahamisha majukumu na utamaduni wa taasisi hii,” alisema Mkemia Mkuu wa Serikali.

Pia, Dkt. Mafumiko ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawawezesha watumishi hao kuijua vyema Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa maana ya majukumu yake nyeti kwa Serikali na jamii ya Watanzania lakini pia watajifunza umuhimu wa utunzaji wa siri ambao ni moyo wa utendaji wa Mamlaka.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Evaclotida Kapinga, amewasihi watumishi wapya kuwa wasikivu kwa kipindi chote cha mafunzo na pia wawe huru kuuliza maswali pale inapolazimu ili kwa pamoja waweze kuelewa namna shughuli zinavyofanyika kwenye taasisi.

Mafunzo hayo yamewezeshwa na wawasilishaji mbalimbali kutoka ndani ya taasisi, wataalam kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) pamoja na wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.