Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WANAWAKE WATAKIWA KUTUMIA FURSA KUJILETEA MAENDELEO

Imewekwa: 09 Mar, 2026
WANAWAKE WATAKIWA KUTUMIA FURSA KUJILETEA MAENDELEO

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataka wanawake nchini kuendelea kujituma katika kazi na kutumia fursa wanazopewa ili kuchangia maendeleo ya taifa pamoja na kujijengea ustawi wao binafsi.

Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Mbande wilayani Kongwa Machi 8, 2026, Senyamule alisema wanawake wanapaswa kutumia ipasavyo fursa za usawa na uwezeshaji zinazotolewa na kuunga mkono waliofanikiwa kiuchumi na kijamii, pia kuwapongeza wakazi wa Mkoa wa Dodoma kwa hatua kubwa waliyoipiga katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Napenda kuwataka kutumia siku hii kuhamasisha kuhusu fursa za haki za uchumi na kuwaunga mkono wanawake walioonesha njia, pia naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza wanaume na wanawake wote wa Mkoa wa Dodoma kwa jitihada wanazofanya katika kupambana na ukatili wa kijinsia. Mwaka 2024 tulikuwa na matukio 17,927 yaliyohusisha wanawake na wanaume, lakini kutokana na juhudi za Serikali na jamii, matukio hayo yamepungua hadi kufikia 8,020 mwaka 2025, sawa na punguzo la takribani asilimia 44.7,” alisema Senyamule.

Kwa upande wao, baadhi ya wanawake kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) wamesema taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika kazi na shughuli za maendeleo.

Happyness Ndegeiswa kutoka Makao Makuu ya Mamlaka  jijini Dodoma alisema uwezeshaji unaotolewa na ofisi yao umewapa wanawake fursa ya kuonyesha uwezo wao katika utumishi wa umma.

“Katika kuadhimisha siku hii ya wanawake duniani, napenda kuipongeza Mamlaka kwa kutujali na kutuwezesha wanawake kushiriki maadhimisho haya kila mwaka. Pia kumekuwa na ongezeko la watumishi wanawake, jambo linaloonesha dhamira ya kuimarisha usawa wa kijinsia kazini,” alisema Ndegeiswa.

Aliongeza kuwa wanawake wanapaswa kuendelea kujituma katika majukumu yao ili kuongeza pato la Taifa pamoja na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao katika malezi ya watoto na ustawi wa familia.

Naye Asanath Ally kutoka Ofisi ya Kanda ya Kati alisema usawa wa kijinsia ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii na ni muhimu jamii kutambua kuwa haki na usawa wa wanawake sio suala lao peke yao bali ni msingi wa maendeleo ya jamii nzima, kwani mwanamke akiwezeshwa ana uwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo ya familia na taifa.

Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka Machi 8, ambapo mwaka huu wa 2026 yalibeba kaulimbiu isemayo: “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana; Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050.”