WATUMISHI WA MAMLAKA WAPIGWA MSASA KUJIKINGA NA MOTO
Watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wametakiwa kuyapa thamani na kufanyia kazi mafunzo ya kinga na tahadhari ya moto kwa kuendelea kutoa elimu hiyo kwa jamii namna ya kujikinga na majanga ya moto.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo Januari 26, 2026, Jijini Dodoma, Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema kuwa ni jukumu la kila mmoja kuelewa mifumo yakuzimia moto na vifaa vinavyotumika kuzima moto pindi majanga yanapotokea wawapo nyumbani au ofisini.
“Kubwa zaidi ninachotaka niwaeleze ni kwamba, tuhakikishe vifaa vinavyoweza kubaini moshi vinafanya kazi. fikiria tumewekeza katika hili jengo pesa nyingi, vifaaa vilivyopo humu ndani ni mabilioni ya hela lakini vyote hivyo tunaweza tukaviteketeza kwa mara moja kwa ajali ya moto ni mbaya. Lingine ninachoweza kusema ni kuwa kama kuna mwenzetu katika kitengo chetu tunachokaa hajahudhuria basi mpe hiyo elimu, tujaribu kugawana hata katika familia, “Alisema Dkt. Mafumiko.
Akizungumzia mafunzo hayo Mrakibu Msaidizi kutoka Jeshi la zimamoto, Stephen Katte, amewataka watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa mabalozi kwa jamii kwa kutoa elimu ya namna ya kujikinga na majanga ya moto.
“Elimu hii nina imani hata kama imefikia watu hamsini, watu mia moja au mia mbili kwa wote hawa tukiwa mabalozi wa kwenda kuelimisha kwa maana dada wa kazi tuliowaacha nyumbani, majirani zetu na watu wengine basi itakuwa ni tija kuendelea kuweka mazingira yetu na nchi nzima kuwa salama kwa ujumla,” alisema Katte.
Kwa upande wao Watumishi wa Mamlaka waliopata mafunzo hayo wameishukuru Mamlaka na Jeshi la Zimamoto kwa kupewa mafunzo hayo na wameahidi kuwa chachu ya kutoa elimu kwa watumishi ambao hawajashiriki mafunzo hayo na kwa jamii inayowazunguka ili kuepuka na kujikinga na majanga ya moto wawapo kazini na nyumbani.