Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WANAWAKE GCLA WATOA MSAADA KWA WATOTO NJITI

Imewekwa: 09 Mar, 2026
WANAWAKE GCLA WATOA MSAADA KWA WATOTO NJITI

Katika kuadhimisha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, 2026, wanawake wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wametoa misaada kwa watoto njiti katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

Akizungumza kwa niaba ya wanawake wa Mamlaka, Mwenyekiti wa Wanawake GCLA, Veronica Chiligati amesema wametoa msaada huo wa mahitaji mbambali kwa lengo la kuwasaidia watoto njiti waliozaliwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam, Machi 6, 2026.

“Kama ilivyo utamaduni wetu wa kurudisha kwa jamii, katika kila mwaka kuelekea Siku ya Wanawake Duniani, wanawake wa Mamlaka huwa tunatembelea wahitaji na kuwafariji kwa kidogo tulichojaliwa. Niwapongeze wanawake wa GCLA kwa kuonesha upendo kwa jamii na kuwaomba kuendeleza tamaduni hiyo”, alisema Chiligati.

Aidha, muuguzi kutoka kitengo cha kuhudumia watoto njiti hospitali ya Taifa Muhimbili, Monica Mtundu amewashukuru wanawake wa GCLA kwa kuonesha upendo kwa watoto hao waliopo chini ya uangalizi.

Kwa upande wao wazazi wa watoto waliopo chini ya uangalizi, wameziomba taasisi, mashirika na makundi mbalimbali kujitokeza kusaidia wenye uhitaji iwapo wataguswa.

Sambamba na hayo, wanawake wa Mamlaka wamewalipia gharama za hospitali kwa zaidi ya wazazi 12 waliokuwa wameshindwa kulipa bili za matibabu ili waweze kuruhusiwa.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani 2026, yenye kaulimbiu “Haki sawa kwa Wanawake na Wasichana, Msingi Jumuishi Kufikia Dira ya 2050” kwa Mkoa wa Dar es Salaam yalifanyika kwenye viwanja vya Mburahati Machi 8, 2026.