Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WATUMISHI WAPYA WA GCLA WASISITIZWA WELEDI KATIKA KAZI

Imewekwa: 16 Apr, 2025
WATUMISHI WAPYA WA GCLA WASISITIZWA WELEDI KATIKA KAZI

Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko, amewataka waajiriwa wapya pamoja na waliohamia katika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kuwa waadilifu na wazalendo katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ndani ya Mamlaka hiyo.

Dkt Mafumiko ameyasema hayo Februari 24, 2025, wakati akifungua mafunzo ya awali kwa waajiriwa hao pamoja na watumishi waliohamia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, mafunzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

“Kama mnavyofahamu kila taasisi ina majukumu na utamaduni tofauti na taasisi nyingine. Hivyo, tunatoa mafunzo haya ili kuhakikisha kwamba watumishi wote wa Mamlaka wanaelewa vyema majukumu ya Mamlaka na hivyo kuwezesha utekelezaji wa majukumu yenye ufanisi zaidi, lakini pia yenye uadilifu na zalendo wa hali ya juu” alisema Dkt. Mafumiko.

Kwa upande wake Meneja wa Fedha na Uhasibu wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu Serikali, Matrida Lugenge, amewasisitiza watumishi hao kuwa chachu ya kuleta matokeo bora katika utendaji kazi wao ndani ya Mamlaka, Serikali na jamii kwa ujumla.

“Ninaamini kipo kitu Serikali inategemea kutoka kwenu, hivyo mnahitajika kupenda kazi, kutunza siri, kuwajibika na kutambua majukumu ya Mamlaka katika kutoa huduma bora zenye matokeo chanya kwa Mamlaka, Serikali na jamii kwa ujumla. alisema Matrida.