WATUMISHI WAASWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUFANYA MAZOEZI

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amewataka watumishi wa Mamlaka kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi na michezo ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza na kuimarisha afya zao.
Mkemia Mkuu wa Serikali ametoa rai hiyo Julai 19, 2025 wakati wa ufunguzi wa Bonanza la watumishi wa Mamlaka, takribani 190 kutoka Makao Makuu, Dodoma na Ofisi ya Dar es Salaam lililofanyika katika eneo la Ndoto Pole pole lililopo Mapinga, Bagamoyo.
“Michezo husaidia kuboresha afya na kujenga mahusiano mazuri kati ya watumishi. Utekelezaji Mzuri wa majukumu yetu ya kila siku hutegemea sana afya ya mwili na akili” alisema.
Aidha, Dkt. Mafumiko, alisema kuwa kupitia michezo watumishi hupata burudani na kupunguza msongo wa mawazo unaoweza kusababishwa na kukosa nafasi ya kufanya mazoezi au kushiriki michezo mbalimbali.
Hata hivyo, alieleza lengo la bonanza hilo kuwa ni kuwapa washiriki fursa ya kufarahia burudani mbalimbali katika mazingira yasiyo rasmi ya kikazi, ili kusaidia kupumzisha akili na kuongeza ari ya utendaji, kuwezesha ushiriki wa michezo na shughuli za mazoezi kwa lengo la kuimarisha afya ya mwili na akili na kutoa jukwaa la kubadilishana mawazo na uzoefu.
Naye mmoja wa watumishi wa Mamlaka kutoka Makao Makuu Dodoma, Msafiri Mwasyeba, alimshukuru Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Menejimenti ya Mamlaka kwa kuweza kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili bonanza la michezo kwa watumishi.
“Bonanza hili kwetu sisi watumishi ni jambo la faraja sana, kwani linaamsha ari ya kazi, kwa sababu tukitoka hapa baada ya michezo tunarudi kazini tukiwa wenye afya, nguvu na ari mpya kwa ajili ya kushiriki katika kazi zetu za kila siku” alisema.
Hata hivyo, alitoa wito kwa uongozi kuendeleza utamaduni wa kuwa na bonanza la michezo kila mwaka ili kuendeleza dhana ya michezo ni afya na pia kuwa nyenzo muhimu ya kujenga ushirikiano baina ya watumishi.
Bonanza hilo lilihusisha michezo mbalimbali kama vile Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete, Mpira wa wavu, kuendesha baiskeli na michezo mbalimbali ya Jadi.
Awali kabla ya kuanza kwa Bonanza Watumishi wa Mamlaka walisimama kwa dakika moja kuwakumbuka watumishi wenzao Wilson Sonelo na Rashid Mjema waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani tarehe 12 Juni, 2025 mkoani Morogoro wakiwa safarini kikazi.