Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WATUMISHI MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI WATOA MSAADA HOSPITALI YA SARATANI YA OCEAN ROAD

Imewekwa: 20 May, 2024
WATUMISHI MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI WATOA MSAADA  HOSPITALI YA SARATANI YA OCEAN ROAD

@gcla_official Ofisi ya Kanda ya Mashariki,  leo Mei 18, 2024 imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vya kujikimu kwa wagonjwa wa saratani, wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) .

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki Bwa. Danstan Mkapa, amesema watumishi wa Mamlaka wamechukua jukumu la kutoa msaada huo ili kuwafariji wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo. 

"Taasisi ya Saratani Ocean Road ni jirani zetu na sisi kama watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, tumeguswa kuja kufanya matendo ya huruma kwa wagonjwa wanaotibiwa hapa, na kuwaunga mkono na kuwafariji katika matibabu wanayopatiwa.

Aidha Mkapa amewapongeza watoa huduma wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, kwa kujitoa kwao ipasavyo katika kuwahudumia wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Taasisi hiyo. 

Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani  Ocean Road, Bi. Christina Tarimo, ametoa shukrani za dhati kwa watumishi wa GCLA kwa kuwaunga mkono katika mapambano dhidi ya Saratani na kwa msaada uliotolewa na kueleza kuwa umeletwa wakati muafaka ukizingatia kwamba matibabu ya Saratani yanachukua muda mrefu kwa wagonjwa kulazwa katika Taasisi hiyo, hivyo vifaa vilivyotolewa vitawasaidia kujikimu katika matumizi ya kila siku.

Mbali na kushiriki kufanya matendo ya huruma kwa wagonjwa wa Saratani wanaotibiwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, pia watumishi wa Mamlaka hiyo kanda ya Mashariki Mei 19, 2024 watakuwa pia na bonanza la pamoja lengo likiwa kuwakutanisha pamoja watumishi wa kanda hiyo na kushiriki michezo mbalimbali.