Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WATUMISHI GCLA WAKUMBUSHWA UADILIFU KAZINI

Imewekwa: 14 Jun, 2025
WATUMISHI GCLA WAKUMBUSHWA UADILIFU KAZINI

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewasisitiza watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufuata Sheria, taratibu na Kanuni za Utumishi wa Umma ikiwemo suala la kuwahi kazini kwa wakati.

Dkt. Mafumiko amesema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Makao Mkuu na Ofisi ya Kanda ya Kati katika kikao kilichofanyika Juni 4, 2025 katika Makao Makuu ya Mamlaka, jijini Dodoma.

“Niwaase watumishi wenzangu tujitahidi kuheshimu taratibu zote zinazotolewa na Serikali kupitia Utumishi, tusijenge tabia ya kuchelewa kazini bila sababu kwani kwa kufanya hivyo ni kosa la kinidhamu na adhabu yake ni kubwa mno. Hivyo tujitahidi kurekebisha mienendo ya mahudhurio mazuri kazini. alisema Dkt. Mafumiko.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Sylvester Omary, amewasihi watumishi hao kujenga tabia ya kutoa taarifa ya kutokuwepo kazini kwa kiongozi husika ili kuepuka changamoto zitakazojitokeza kutokana na kutotoa taarifa kwa wakati.

“Niwasihi watumishi wenzangu kutokana na mfumo tulionao sasa wa kiutumishi wa mahudhurio kazini unahitajika kutoa taarifa pindi unaposafiri kikazi au kama umepatwa na changamoto yoyote, kutoa taarifa ya kimaandishi kwa kiongozi wako itasaidia kuweka kumbukumbu ili panapotokea changamoto itasaidia kuweka mambo sawa kupitia taarifa zako hizo” alisema Omary.