Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WATAALAM WA MAABARA WAHIMIZWA KULINDA ITHIBATI

Imewekwa: 16 Jan, 2026
WATAALAM WA MAABARA WAHIMIZWA KULINDA ITHIBATI

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imetoa mafunzo ya utekelezaji wa mifumo ya ubora ya maabara (ISO/IEC 17025:2017) kwa wataalam wa maabara kwa lengo la kuongeza umahiri katika utendaji wa kila siku katika maabara, kuongeza umahiri kwa watumishi, kuimarisha hadhi ya maabara za Mamlaka kulingana na Viwango na matakwa ya Kimataifa pamoja na kuiwezesha Mamlaka kuongeza wigo wa Ithibati katika Maabara zake.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika Januari 5 hadi 9, 2026 kwenye Chuo cha Ustawi wa Jamii, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amesema kiwango cha ISO/IEC 17025:2017 kinaipa maabara uwezo wa kuonesha umahiri wake katika kufanya uchunguzi na kutoa matokeo ya maabara yanayotambulika na kukubalika kitaifa na kimataifa, na utekelezaji wa kiwango hicho si hitaji la ithibati pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kuimarisha ubora, uaminifu na ushindani wa huduma za maabara.

“Nitumie fursa hii kusisitiza kwamba juhudi na uwajibikaji wenu ndiyo msingi wa mafanikio ya ithibati katika Mamlaka. Mafanikio ya Maabara kupata ithibati na kuitekeleza kwa vitendo yatatoa sifa njema si tu kwa Mamlaka bali pia kwa Taifa kwa ujumla. Aidha, Mamlaka itaendelea kutoa rasilimali zinazohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa ubora ulioanzishwa kulingana na mahitaji ya viwango vya Ubora wa Kimataifa (ISO),” alisema Dkt. Mafumiko.

Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali ametoa msisitizo kwa watumishi wote wa Mamlaka kuhusu umuhimu wa kuwajibika binafsi na kujitambua kitaaluma, hususan kadri mtu anavyozidi kupata uzoefu katika maeneo yake ya kazi kwani uzoefu wanaoupata si mali ya mtu binafsi pekee, bali ni rasilimali muhimu ya Taasisi inayopaswa kushirikishwa na kuendelezwa kwa makusudi ili kujenga uwezo endelevu wa Mamlaka.

Kwa upande wake Mwezeshaji kutoka Umoja wa Maabara, Bi. Kezia Mbwambo amesema kuwa Kiwango cha ISO/IEC 17025:2017 ni mfumo wa usimamizi uliotengenezwa na Shirika la Viwango vya Kimataifa (ISO) linalolenga seti ya mahitaji ambayo Taasisi au Shirika linapaswa kufikia katika mfumo wa ubora ili kupata hati ya ISO.

Naye Riphat Lusingo, ameishukuru Mamlaka kwa kuwezesha mafunzo hayo na kuahidi kwa niaba ya wataalam wote wa maabara kuendelea kujituma katika kutekeleza mifumo ya ubora kwa kuzingatia matakwa ya viwango vya kimataifa vya maabara, kutekeleza taratibu, miongozo na nyaraka za maabara kwa hiari na uwajibikaji.