Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WANAFUNZI WATAKIWA KUTUMIA FURSA KWENYE ELIMU

Imewekwa: 14 Jun, 2024
WANAFUNZI WATAKIWA KUTUMIA FURSA KWENYE ELIMU

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) Imetoa zawadi kwa wanafunzi na walimu waliofanya vizuri zaidi kitaifa kwenye masomo ya Kemia, Fizikia na Baiolojia kidato cha Nne, 2022 na Kidato cha sita 2023.

Akizungumza wakati wa kutoa zawadi hizo Juni 7, 2024 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu amesema kuwa wanafunzi hao wanastahili pongezi kwa kufanya vizuri zaidi kitaifa katika masomo ya sayansi na kutumia vizuri fursa ambayo Serikali imewekeza katika sekta ya elimu nchini.

“Wanafunzi mmefanya vizuri katika masomo yenu na ndiyo maana leo hii tupo hapa kwa lengo moja tu la kuwapongeza kwa sababu mmefanya jambo kubwa, jambo zuri. Mnastahili pongezi, huu uwekezaji ambao Rais Samia anaendelea kufanya kwenye sekta zote, sasa nyie mmetumia fursa hiyo vizuri na leo tunawapongeza” alisema.

 Dkt. Jingu, alisema kuwa Sayansi ni dunia ya leo na ya kesho na ndiyo inayotoa majawabu ya mambo makubwa ya mustakabali wa maisha yetu, iwe kwenye kilimo, ufugaji, afya na mengineyo. Amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika maeneo ya sayansi, uwekezaji mkubwa kuanzia shuleni hadi kwenye vyuo vya mafunzo ili wanafunzi waive vizuri na kuwa mahiri na kuleta majawabu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.

Akizungumza kuhusu Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Jingu alisema kuwa GCLA ni chombo muhimu  sana katika Maisha ya nchi yetu na  pia kwenye sekta ya afya  ni moja ya nguzo kubwa na kwenye mnyororo wa haki jinai husaidia vyombo vinavyohusika na utoaji wa  haki jinai, kutenda kazi zao vizuri katika kuleta  haki na kwa jamii husaidia  kupata majawabu ya kisayansi,

“Natoa wito kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuendeleza zoezi hilo na kuongeza ubunifu wa mara kwa mara wa kuwazawadia wanaofanya vizuri na kuendelea kushirikiana na watoa mafunzo ili mwisho wa siku jamii iweze kuchangia kupata wanasayansi walioandaliwa vizuri na wenye kutoa majawabu” alisema Katibu Mkuu.

Vile vile ametoa wito kwa wadau wengine kuongeza nguvu na uwekezaji kwenye maeneo ya sayansi ili wanasayansi wetu wapate mazingira mazuri ya kusoma.

“Ni muhimu sana tuendelee kuwekeza katika eneo la sayansi, tuwe na wanasayansi mahiri ambao watajibu masuala makubwa ambayo yanayosumbua maisha yetu katika nyanja mbalimbali, kwani dunia ya leo na dunia ya kesho itatanabainishwa na sayansi, kwa hiyo lazima tuendelee kuwekeza katika maeneo ya sayansi”.

Aidha, aliwashukuru wazazi na walezi kwa malezi mazuri kwa vijana hao na kueleza kuwa malezi ndiyo yanaamua mustakabali wa mtoto achukue mkondo upi wa maisha. Amesisitiza kuwa wazazi ndio wanaotengeneza dunia na ikiwa wazazi wataacha kutimiza wajibu wao kama walezi matokeo yake ni kupata watu katika jamii wanaokuwa mzigo, amewasisitiza wazazi kuwekeza kwenye maadili mazuri kwa watoto wao ikiwa ni pamoja na kupenda kufanya kazi na kuwa na tabia njema.

Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema, jumla ya wanafunzi 384 wametunukiwa vyeti tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo mwaka 2007 na walimu 48 wamepongezwa. Amesema, Mamlaka ina mpango wa kuongeza kuwatunuku wanafunzi watakofanya vizuri zaidi kitafa katika somo la Hisabati kuanzia 2025.

Naye Munge Daniel, mwakilishi wa Wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa katika masomo ya Sayansi akiongea kwa niaba ya wanafunzi  wenzake amesema kuwa pongezi na zawadi hizo zimewapa motisha kubwa sana kwao kwa vile zinawapa hamasa kuendelea kupigania ndoto zao ziweze kuishi, na pia zinawapa hamasa wadogo zao na wanafunzi wengine kufanya bidii ili nao wafikie hatua kama yao.

Mwakilishi wa Wazazi ambaye pia ni Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Nenelwa Mwihambi, akiongea kwa niaba ya wazazi wa watoto waliofanya vizuri zaidi kitaifa kwenye masomo ya sayansi ameishukuru Serikali kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa wazo hilo zuri na ubunifu huo ambao amesema unaleta motisha kubwa sana kwa Watoto na kwa wazazi pia. Aidha, amewashukuru wanafunzi hao kwa kuwaheshimisha na pia amewashukuru walimu kwa kuwawezesha wanafunzi hao kufikia hatua hiyo.