Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

GCLA YATAMBULIKA KIMATAIFA KATIKA UTOAJI HUDUMA

Imewekwa: 28 Jan, 2026
GCLA YATAMBULIKA KIMATAIFA KATIKA UTOAJI HUDUMA

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imetunukiwa Cheti cha Heshima cha Forodha kwa kuthamini na kutambua mchango wake na utoaji huduma wa kipekee kwa jumuiya ya kimataifa ya Forodha.
 

Cheti hicho kimetolewa na Shirika la Forodha Duniani kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Forodha 2026 yaliyofanyika Januari 26, 2026, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kabla ya kukabidhi cheti hicho, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, ameipongeza GCLA kwa ushirikiano wake wa karibu na wa muda mrefu na TRA, uliosaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha ufanisi wa shughuli za forodha bandarini, kurahisisha biashara na kuimarisha udhibiti wa mapato ya Serikali.

“Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeendelea kuwa mdau muhimu na mfano wa kuigwa kwa kuzingatia misingi ya weledi, uwajibikaji na uadilifu, huku ikiendelea kushirikiana kwa karibu na TRA katika utekelezaji wa maboresho ya mifumo na taratibu za forodha kwa manufaa ya taifa” alisema Kamishna Mwenda.

Akipokea Cheti hicho kutoka kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, kwa niaba ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa, ameishukuru TRA na Utawala wa Forodha wa Tanzania kwa kutambua mchango wa GCLA na kuahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo ili kuongeza ufanisi wa bandari na kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Forodha 2026 yalilenga kutambua na kuenzi mchango wa sekta ya forodha katika kukuza biashara halali, kulinda uchumi wa taifa, kuongeza makusanyo ya mapato ya Serikali, pamoja na kuimarisha uwajibikaji na ushirikiano kati ya TRA na wadau wake wakuu, wakiwemo taasisi zinazosimamia bandari na biashara ya kimataifa.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt. Ashura Katunzi, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru.