WADAU WATAKIWA KUZINGATIA MATUMIZI YA KEMIKALI BASHIRIFU

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imewakumbusha wadau wanaojihusisha na shughuli za kemikali kuhakikisha wanazingatia matumizi salama ya kemikali na kutojihusisha na uchepushwaji wa kemikali bashirifu kwa ajili ya utengenezaji wa dawa za kulevya.
Akizungumza Mei 28, 2025, jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao hicho Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, amewataka wadau wa kemikali kushirikiana na Mamlaka za Udhibiti ili kutokomeza uchepushwaji wa kemikali bashirifu kwa ajili ya matengenezo ya dawa za kelevya kwani dawa za kulevya huleta athari za kiuchumi, nguvu kazi na kuporomoka kwa maadili.
“Nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa inatokomeza uingiaji, utengenezaji na matumizi ya dawa za kulevya nchini. Hata hivyo, ili lengo hilo liweze kutimia ni lazima kuziba mianya yote inayochangia masuala hayo kufanyika, na wenye kufanikisha hilo ni kila mmoja wetu. Endapo tutatimiza wajibu wetu ipasavyo, hili linawezekana endapo wote tutakuwa na nia ya pamoja katika kutimiza wajibu wetu,” alisema Dkt. Mafumiko.
Naye, Kamishna wa Ukaguzi na Sayansi Jinai kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Domician Mutayoba amesema kupitia Mamlaka za Udhibiti wanahakikisha wanatengeneza ushirikiano ulio imara kwa kuwa na jumuia ambapo kupitia jumuia hiyo, wadau wataweza kutengeneza utaraatibu muhimu katika muktadha mzima wa kudhibiti na kuzuia uchepushwaji wa kemikali bashirifu zisitumike katika utengenezaji wa dawa za kulevya na silaha.
Kwa upande wake Meneja wa Total Med-Lab Solutions, Shaphii Miraji ameishauri Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa kemikali kwani teknolojia inabadilika hivyo elimu iendelee kutolewa ili kuzidi kuboresha masuala ya kemikali nchini.