Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WADAU WATAKIWA KUWA NA UELEWA WA KEMIKALI

Imewekwa: 14 Jun, 2024
WADAU WATAKIWA KUWA NA UELEWA WA KEMIKALI

Taasisi za Umma na binafsi zimetakiwa kutenga bajeti Kwa ajili ya kuwawezesha wataalam wanaojishughulisha na masuala ya kemikali kuendelea kupata elimu sahihi ya matumizi salama ya  kemikali ili kulinda Afya zao pamoja na mazingira.

Akizungumza mkoani Kigoma katika mafunzo ya kuwajengea uelewa wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali kwa taasisi za umma na wadau wa kemikali, Mkurugenzi wa huduma za Udhibiti kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Daniel Ndiyo, amesema wataalam hao wanapokuwa na elimu sahihi kuhusu kemikali watailinda jamii yote na watanzania kwa ujumla na kuwa nafasi kubwa ya kufanya kazi.

"Niziombe Taasisi za Umma, binafsi pamoja na waajiri wengine wote ambao wanajihusisha na masuala ya kemikali wajitahidi kutenga bajeti Kwa ajili ya kuwawezesha wataalam wa kemikali kupata elimu sahihi Kwa sababu mtu anapokuwa na elimu sahihi kuhusiana na matumizi ya kemikali atamlinda mwenzake, atailinda jamii ya watanzania, vile vile atajilinda yeye mwenyewe anapotekeleza majukumu yake"alisema Daniel Ndiyo.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, katika mafunzo hayo, Katibu Tawala Msaidizi wa Biashara na Uwekezaji Kigoma, Deogratius Sangu, amewataka wadau hao kusimamia Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Namba 3 ya Mwaka 2003, pamoja na Kanuni zake za Mwaka 2020, pindi wanapotekeleza majukumu yao.

"Ndugu washiriki Mkoa wa Kigoma ukiwa ni sehemu ya nchi hii na ukiwa na bandari za kuingiza au kutoa shehena za kemikali nchini, nao pia unaguswa na matakwa ya Sheria hii"alisema Deogratius Sangu.

Kwa upande wake mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Gwakisa Maseba, amesema mafunzo hayo yameongeza uwezo na ari ya kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuimarisha ushirikiano na wataalamu wa kemikali.

"Kwetu sisi mafunzo haya yametuongezea uwezo na ari ya kufanya kazi, lakini pia kuona jinsi ambavyo tutaweza tukashirikiana na wataalamu wa kemikali na hata wataalamu kutoka idara nyingine katika maeneo yetu ya kazi ili kuona kwamba tunafanya hivyo katika kutekeleza wajibu wetu na pia kuzingatia Sheria na taratibu zote zinazohusiana na kemikali zinafuatwa" alisema Gwakisa.