Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WADAU WASISITIZWA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI

Imewekwa: 06 Dec, 2025
WADAU WASISITIZWA MATUMIZI SALAMA YA KEMIKALI

Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Kanda ya Kaskazini, Eliamini Mkenga, amewataka wasimamizi na watumiaji wa kemikali kutumia kwa uangalifu kwa sababu hakuna kemikali rafiki kwa binadamu na mazingira.

Meneja Mkenga amesema hayo Desemba 2, 2025 wakati akifungua mafunzo ya usimamizi salama wa kemikali kwa wasimamizi wa kemikali kutoka kampuni ya gesi ya Gasco na wadau wengine wa kemikali kutoka jijini Arusha.

“Hakuna kemikali rafiki kwa binadamu, kila moja ina madhara kwa binadamu kama itatumiwa tofauti na inavyotakiwa kulingana na maelekezo yake. Hivyo tunahitajika kuwa waangalifu na makini tunapotumia na kuzisimamia kemikali za aina yoyote. Mafunzo haya yatawasaidia kuweza kufahamu namna ya kutunza, kusafirisha na kujikinga ili kutoweza kupata madhara ya kemikali mnapokuwa mnazitumia na kuzisimamia” alisema Mkenga.

Aidha, alieleza kwamba Sheria inawataka kutoa mafunzo kwa wasimamizi na watumiaji wa kemikali mara kwa mara ili kuongeza umakini na kuchukua tahadhari ya matumizi ya kemikali kwenye maeneo ya kazi.

“Lazima tuzingatie taratibu za usalama wa matumizi ya kemikali ili kuepusha ajali na madhara yanayoweza kusababishwa na kemikali zisiposimamiwa kikamilifu” alimaliza Meneja Mkenga.

Naye mshiriki wa mafunzo hayo kutoka kampuni ya Gasco, Lucas Godfrey, akiongea kuhusu mafunzo hayo alisema mtazamo wao mkubwa walionao ni kwamba mafunzo hayo yatawaongezea uelewa katika matumizi ya kemikali lakini pia kujua mabadiliko na maboresho ya miongozo na sheria ya kemikali ili kuhakikisha wanawajibika katika usimamizi wa kemikali.

“Mafunzo haya ni sehemu ya kuboresha katika mapungufu tuliyonayo hususani katika eneo la kemikali kwenye uhifadhi na matumizi lakini pia kufikisha elimu hii kwenye maeneo yetu ya kazi na jamii husika” alimaliza Godfrey.