WADAU WA MAFIA WAPATA ELIMU YA VINASABA NA KEMIKALI

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki imetembelea wanafunzi na walimu wa shule mbalimbali za sekondari zilizopo wilaya ya Mafia na kuwapa elimu kuhusu masuala ya huduma za Vinasaba ikiwemo upatikanaji wa haki kwenye makosa ya jinai kama ya ubakaji, ulawiti pamoja na kufahamu matumizi ya kemikali na madhara yake.
Akizungumza baada ya kukamilisha mafunzo hayo yaliyofanyika kuanzia Aprili 8 hadi 10, 2025, Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa amesema dhumuni la kufikisha elimu hiyo ya Vinasaba na Kemikali kwa wanafunzi ni kuhamasisha wanafunzi kupenda kusoma masomo ya sayansi na kuwa mabalozi katika kuelimisha jamii inayowazunguka kuhusu vinasaba na matumizi salama ya kemikali.
“Kupitia elimu hii ya vinasaba, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali inaamini kwamba wanafunzi hawa tayari wana uelewa juu ya nini cha kufanya endapo mwanafunzi au mwenzake amekumbwa na tatizo la ubakaji au ulawiti pamoja na kutatua changamoto za ajali za kemikali wakiwa mashuleni au majumbani,” alisema Mkapa.
Kwa upande wake Afisa Elimu Maalum Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Musa Abdallah, ameishukuru Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuwafikia wanafunzi ambao ndio walengwa wa masuala mbalimbali yanayotokea katika jamii lakini pia kuwa viongozi na wanasayansi wa baadae.
Naye mwalimu wa masomo ya sayansi katika shule ya sekondari Baleni, Eddy Mjige amesema kuwa ujio wa wataalam kutoka GCLA utakuwa na manufaa makubwa kwa walimu wa masomo ya sayansi hasa katika zoezi la uendeshaji wa maabara na matumizi yaliosahihi ya kemikali kwenye maabara wakati wa elimu kwa vitendo.
Sambamba na hayo, mwanafunzi kutoka shule ya sekondari Kilindoni, Yahya Hafidhi, ameiomba Mamlaka kuendelea na utoaji wa elimu kuhusu majukumu yake na mbinu za kuwawezesha wanafunzi kutoa elimu kwa jamii inaowazunguka.