Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WADAU WA KEMIKALI WAHIMIZWA KUFAHAMU SHERIA ZA KEMIKALI

Imewekwa: 14 Dec, 2023
WADAU WA KEMIKALI WAHIMIZWA KUFAHAMU SHERIA ZA KEMIKALI

Wadau wanaojihusisha na masuala ya usafirishaji, uingizaji, utumiaji na usambazaji wa kemikali nchini wahimizwa kuzifahamu vizuri Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali pamoja na Kanuni zake za mwaka 2020.

Hayo yamesemwa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko amesema hayo Disemba 8, 2023 wakati akifunga Mafunzo ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali yaliyofanyika kwa siku tatu katika ukumbi wa Mount Meru Hoteli jijini Arusha.

“Mamlaka inaamini kwamba baada ya mafunzo haya, wadau hawa wataweza kufahamu Sheria inataka nini na Kanuni zinazosaidia utekelezaji wa majukumu zinawataka wafanye nini kama wadau muhimu sana kwenye sekta ya kemikali, ili pale watapokuwa wanakidhi matakwa basi itasaidia kuchochea biashara zao na hivyo uwezeshaji wa Mamlaka kwenye biashara ya kemikali unakuwa rahisi,” alisema Dkt. Mafumiko.

Dkt. Mafumiko ameongeza kuwa kemikali zina manufaa mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi na kwa wanaojishughulisha nazo kwani kuna kemikali za aina tofauti tofauti ambapo amesema kuna kemikali ambazo hazina madhara makubwa na kemikali ambazo tabia zake zinaweza kuwa na madhara makubwa sana kama hazitatumika kwa usahihi na usalama.

Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali amesema kuwa lengo kuu la msingi la mafunzo hayo ya usimamizi wa kemikali ni kulinda afya ya mwananchi pamoja na mazingira yake, hivyo ni wajibu wa kila mdau wa kemikali kuhakikisha anasimamia vyema masuala ya usalama mahala pa kazi kwa wafanyakazi na kwa mazingira.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Magdalena Mtenga amesema kuwa Mamlaka itaendelea kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kemikali kwa wadau tofauti tofauti wakiwemo wajasiriamali wadogo wa kemikali ili kuepusha athari ambazo zinaweza kutokea endapo matumizi ya kemikali hayatazingatiwa.

Kwa upende wake mshiriki wa mafunzo, Christian Sebastian amesema kuwa baada ya kupata mafunzo ya usimamizi na udhibiti wa kemikali, anaamini mafunzo hayo yataendelea kuwajenga na kuwakuza kwenye ufanisi katika mausuala mazima ya utendaji kazi haswa katika shughuli za kemikali pamoja na kuongeza ushirikiano zaidi baina na wadau na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA).

Mafunzo hayo yameandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki na Kanda ya Kaskazini na kushirikisha wadau 148 kwa lengo la kuwajengea uwezo wasimamizi hao wa kemikali.