Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

WADAU NJOMBE WAPATIWA ELIMU USIMAMIZI WA SAMPULI JINAI

Imewekwa: 25 Jun, 2025
WADAU NJOMBE WAPATIWA ELIMU USIMAMIZI WA SAMPULI JINAI

Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe, limeipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kwa kuwapatia mafunzo ya usimamizi wa sampuli za jinai kwa kuwa mafunzo hayo yatawasaidia katika kupambana na uhalifu mkoani humo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Uchunguzi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Njombe, Mrakibu wa Polisi, Siphael Mungure, katika mafunzo ya uchukuaji, Ukusanyaji, Utunzaji na Usafirishaji wa Sampuli za Jinai kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi na Wapelelezi yaliyofanyika mkoani Njombe, Juni 20, 2025.

“Tunaishukuru sana Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutupatia mafunzo haya kwa sababu mafunzo haya yatatusaidia sana katika kupambana na uhalifu katika mkoa wetu, lakini pia yatatusaidia katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku kwa weledi na ufanisi zaidi”. alisema Mrakibu, Mungure.

Kwa upande wake Meneja wa Maabara ya Sayansi Jinai Baiolojia na Vinasaba, Dkt. Fidelis Bugoye, alisema lengo la mafunzo hayo ni utekelezaji wa sheria wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ya mwaka 2016, lakini pia sheria ya Vinasaba vya Binadamu, ambapo Mkemia Mkuu wa Serikali anafanya kazi kwa karibu na wadau wakiwemo Jeshi la Polisi.

“Katika masuala ya jinai, sisi kama Taasisi tuna wajibu wa kufanya uchunguzi na kutoa majibu ambayo yanawasaidia wadau katika kufanya maamuzi katika mashauri mbalimbali kwenye mnyororo wa haki jinai. Na kwa Jeshi la Polisi wana wajibu wa kuchukua sampuli zilizo bora kufungasha na kuziwekea alama ili ziweze kufika Maabara zikiwa kwenye ubora ule ule ambapo zinaweza kutumika na kupata matokeo sahihi, kwa hiyo tumewakumbusha wajibu wao Jeshi la Polisi lakini pia na majukumu yao katika uchukuaji wa sampuli.” Alisema Dkt. Bugoye.