Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

NPCC YAKUTANA NA WASIMAMIZI WA VIWANDA

Imewekwa: 06 Dec, 2025
NPCC YAKUTANA NA WASIMAMIZI WA VIWANDA

Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu (NPCC), imekutana na kuongea na Wakuu na Wasimamizi wa Viwanda walivyovitembelea katika ziara yao iliyofanyika Novemba 11-14, 2025 katika wiki ya kuzuia sumu ya madini ya risasi duniani, lengo kuu likiwa ni kuleta usalama katika afya za watu na mazingira kwa ujumla.

Hayo yameelezwa Desemba 2, 2025 na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Bidhaa na Mazingira, Dkt. Peter Shimo, wakati akizungumza na Wakuu pamoja na Wasimamizi wa viwanda hivyo katika ukumbi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), jijini Dar es Salaam. Huku akiwasihi kuwa makini katika uzalishaji viwandani kwa kufuata kanuni na sheria zilizowekwa ili kuleta usalama wa wafanyakazi viwandani na pia katika mazingira kwa ujumla na mwisho kufanikisha suala zima la kudhibiti matukio ya sumu, hasa katika kuzuia sumu ya madini ya risasi.

“Ziara hiyo ilikuwa imepangwa ili kutoa elimu kwa jamii na kuipa uelewa jamii kwa ujumla juu ya Madhara yanayoletwa na sumu ya madini ya risasi ili kuweza kuokoa maisha ya watu na mazingira, kwasababu katika uchakataji wa betri katika viwanda vyetu kuna uwezekano mkubwa kuwepo kwa madini haya ya risasi” alisema Dkt. Shimo.

Aidha, amewasihi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali pindi wanapokumbana na changamoto yoyote katika viwanda vyao ili kuendelea kulinda afya za jamii na Mazingira.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaalam ya Kudhibiti Matukio ya Sumu ya GCLA, Prof. Amos Mwakigonja, amewataka Wakuu na Wasimamizi wa viwanda hivyo wahakikishe Wafanyakazi wao katika viwanda wanapata vifaa maalum vya kujikinga  wakati wa uchakataji ili kuepusha madhara kwa afya zao. Vifaa hivyo ni pamoja na kuwapa viatu maalumu vya viwandani, mavazi na pia barakoa lengo kuu likiwa ni kuepusha madhara ya sumu ya madini ya risasi.

Prof. Amos Mwakigonja, alibaini kuwa Wafanyakazi wa viwanda hivyo hawapo salama kwa sababu ya kukosa vifaa maalum vya kujikinga wakati wa uchakataji pindi wanapofanya kazi, hali inayopelekea uwezeakano mkubwa wa kupata madhara yanayosababishwa na sumu ya madini ya risasi.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Jane Marwa, ametoa ushauri kwa Wakuu na Wasimamizi hao wa viwanda kuwa wanapaswa kuhakikisha usalama zaidi katika kuwalinda Wafanyakazi wao wa viwandani ili kuepusha madhara yanayosababishwa na sumu ya madini ya risasi.  Amewashauri wao ndio wakawe mfano wa kuigwa kwa Wafanyakazi wao ili kutekeleza agizo la Serikali katika suala zima la kuhakikisha uasalama mahali pa kazi kwa Wafanyakazi hao.

Kwa upande wao Wakuu na Wasimamizi wa viwanda hivyo, wameweza kuishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia kituo cha Taifa cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu (NPCC), kwa kuweza kuendelea kutoa elimu kuhusiana na madhara ya sumu ya madini ya risasi kwa kufanikisha kuweza kutembelea Viwanda vyao na kuwapa uelewa wa madini hayo sambamba na athari za madini hayo. Hivyo wameahidi kwenda kutekeleza yale waliyoyapokea katika kikao hicho.