Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MMS: ELIMU YA KEMIKALI INAWAFIKIA WADAU WETU

Imewekwa: 01 Oct, 2025
MMS: ELIMU YA KEMIKALI INAWAFIKIA WADAU WETU

Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema elimu inayotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa wadau wake kuhusu Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali  imewafikia kwa kiasi kikubwa.

Dkt. Mafumiko ameyasema hayo Septemba 26, 2025 wakati alipotembelea wadau mbalimbali katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika mkoani Geita kuanzia Septemba 18 hadi Septemba 28, 2025.

“Nikiangalia Maonesho haya baada ya kutembelea na pia kuweza kuongea na Wadau wetu hususan wadau wa Kemikali, naona kuna ukuaji mkubwa sana wa uelewa wa wadau juu ya huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, zikiwemo huduma za Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali, lakini pia huduma za uchunguzi wa kimaabara.

Na kwa huduma za Usimamizi wa kemikali ukiacha tu kwamba ule ni uelewa wa wadau lakini na washiriki wanaoshiriki kwenye Maonesho haya baada ya kuongea nao unaona wanaielewa Mamlaka na hata maswali wanayouliza unaona ni ya kujenga zaidi kwa maana ya kuongeza ufanisi, lakini pia na yale masuala ya msingi yanayohusiana na mahitaji ya Sheria mengi wanayatimiza, na hii kwetu sisi kama Mamlaka ambao tunasajili na tunasimamia tunaliona kwa usalama wa watumiaji ni jambo kubwa” alisema Dkt. Mafumiko.

Kwa upande wao baadhi ya wadau wa Mamlaka, Happiness Shumbusho kutoka Jema Africa na Saad Hussein kutoka Waja Chemicals wameishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuwapatia elimu na mafunzo mbalimbali hususan katika maswala ya Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali.

“Sisi kama waingizaji wa kemikali GCLA wametusaidia kwa asilimia kubwa, kwanza tumeweza kupata mafunzo ya moja kwa moja kuhusu masuala ya Udhibiti wa kemikali ambapo kwa sasa matatizo yote yanayohusiana na Kemikali hayapo, Lakini pia kwa upande wa udhibiti wa Kemikali tumekuwa tukielimishwa kuhusu kukata vibali husika na kwa muda sahihi. Pia, GCLA wametusaidia tunapoomba vibali vinakuja kwa wakati” walisema wadau hao.

Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yalianza Septemba 18, 2025 na kuhitimishwa Septemba 28, 2025 huku yakibeba kauli Mbiu Isemayo “Ukuaji wa Sekta ya Madini ni Matokeo ya Matumizi ya Teknolojia sahihi na Uongozi Bora, Shiriki Uchaguzi Mkuu 2025.