Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MAMLAKA YA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI

GCLA Logo
ISO 9001:2015 Certified

MMS AFUNGUA KIKAO KAZI CHA KUTAMBUA VIHATARISHI NA FURSA ZA MPANGO MKAKATI WA MAMLAKA

Imewekwa: 15 Dec, 2023
MMS AFUNGUA KIKAO KAZI CHA KUTAMBUA VIHATARISHI NA FURSA ZA MPANGO MKAKATI WA MAMLAKA

Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko, amefungua Kikao Kazi cha kutambua na kubaini vihatarishi na fursa zinazotokana na Mpango Mkakati wa Mamlaka kinachofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa ADEM uliopo Bagamoyo, Mkoa wa Pwani Disemba 14, 2023.

Dkt. Mafumiko amemtaka kila mshiriki wa kikao hicho kinachofanyika kwa siku mbili, kushirikiana na watumishi wenzake na kiongozi wake katika kuendelea kutambua, kuchambua na kuchanganua kwa usahihi wa vihatarishi na fursa ili ziweze kuwasilishwa kwenye Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi kwa maamuzi.

Aidha, Mkemia Mkuu wa Serikali amesema kuwa taarifa zinazotokana na utekelezaji wa mpango wa usimamizi wa vihatarishi na fursa katika mahala pa kazi ni nyaraka muhimu zinazotumika katika ukaguzi na katika upimaji wa utendaji kazi.

”Kikao hiki ni muhimu kwa kuwa kinazidi kukuza uelewa kwa watumishi wetu na kusaidia Mamlaka kuweza kufikia malengo yake ya kimkakati bila kukabiliana na vikwazo lakini pia kuongeza uwezo wa kutambua fursa ambazo zitaleta tija na maendeleo ya Mamlaka,” amesema Dkt. Mafumiko.

Pia, ameongeza kuwa kazi ya utekelezaji wa usimamizi wa vihatarishi na fursa ambao ni utekelezaji wa sera ya usimamizi wa vihatarishi ya Mamlaka iliyoidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi Juni, 2021, kutokana na maelekezo ya Waraka wa Serikali Na. 12 wa mwaka 2012/2013, uliotolewa na Katibu Mkuu – Hazina.

Dkt. Mafumiko alimalizia kwa kusema kuwa Mamlaka itaendelea kutoa mafunzo na anaamini kuwa washiriki wa kikao hicho watatumia ujuzi, maarifa watakayopata kuboresha, utambuzi, uchambuzi na uchanganuzi wa vihatarishi na fursa katika maeneo ya kazi.